Watu 600,000 hawana chakula Burundi | Masuala ya Jamii | DW | 16.11.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Watu 600,000 hawana chakula Burundi

Kiasi ya watu 600,000 wanakabiliwa na uhaba wa chakula nchini Burundi kutokana na ukame na mafuriko katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita na idadi hiyo inaweza kuongezeka hadi kufikia 700,000 kwa mwaka ujao.

 

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani-WFP, limesema wengi wa walioathirika wanapatikana kwenye majimbo matano ya kaskazini na mashariki mwa Burundi, ambako kiasi ya watu 65,000 wameripotiwa kuvikimbia vijiji vyao.

Mwakilishi wa WFP nchini Burundi, Charles Vincent amesema tatizo hilo linatisha hasa kaskazini mwa Burundi, ingawa amesita kusema kama kuna baa la nja na badala yake kuiita hali hiyo uhaba mkubwa wa chakula. Vincent ametoa matamshi hayo baada ya maafisa wa WFP, Shirika la Kilimo na Chakula Duniani-FAO, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia watoto-UNICEF, pamoja na serikali kuzuru maeneo yaliyoathiriwa kati ya Novemba mosi hadi 3.

Burundi Cibitoke Menschen Alltag Markt (DW/K. Tiassou)

Watu wakinunua vyakula Cibitoke, Burundi

Kati ya Septemba mwaka 2015 na mwezi Mei, Burundi imekumbwa na mafuriko yaliyosababishwa na hali ya El-Nino na baada ya hapo ilishuhudia ukame kutokana na La Nina. Kwa sasa WFP inagawa chakula kwa familia zipatazo 13,000 ambao ni sawa na watu 65,000, katika kukabiliana na tatizo hilo, ingawa imesema juhudi hizo hazitoshi.

Tatizo la uhaba wa chakula linaongeza changamoto zinazoikabili nchi hiyo yenye idadi ya watu milioni 11, ambayo imekuwa kwenye mzozo wa kisiasa na kuhushudia ghasia zilizodumu kwa zaidi ya mwaka mmoja. Mzozo huo ulichochewa na uamuzi wa Rais Pierre Nkurunziza kutangaza kwamba atagombea urais kwa muhula wa tatu.

Mashirika ya haki za binaadamu yaitolea wito jumuiya ya kimataifa

Hayo yanajiri wakati ambapo makundi ya kutetea haki za binaadamu duniani, yametoa wito kwa viongozi wa bara la Afrika, Ulaya pamoja na Marekani kupeleka kikosi cha ulinzi wa raia kwa ajili ya kuzuia uwezekano wa kutokea vita vya wenyewe kwa wenyewe na mauaji ya kimbari.

Shirikisho la Kimataifa la Haki za Binaadamu linalojulikana kana FIDH na Muungano wa Mashirika ya Haki za Binaadamu nchini Burundi-ITEKA, wamesema katika ripoti yao iliyotolewa jana kwamba uamuzi wa hivi karibuni wa serikali ya Burundi kuvunja uhusiano wake na jumuiya ya kimataifa, unaongeza ukandamizaji mpya na uhalifu dhidi ya wananchi ambao wanachukuliwa kama wapinzani wa serikali.

Burundi Polizeigewalt - Polizei schlägt Jungen (picture-alliance/dpa/D. Kurokawa)

Polisi wa Burundi wakimdhibiti kijana mmoja

Ripoti hiyo yenye kurasa 200 inaelezea kile ilichokiita vitendo vya ghasia vinavyofanywa na serikali ya Burundi, ikiwemo kujiondoa katika Mahakama ya Uhalifu wa Kivita-ICC, kuikataa ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu, kukataa juhudi za kutafuta amani za Umoja wa Afrika na maafisa watatu wa Umoja wa Mataifa pamoja na kuyasimamisha mashirika yanayotetea haki za binaadamu, ikiwemo ITEKA.

Utafiti wa ripoti hiyo uliochukua miezi 24, umebaini jinsi serikali ilivyofadhili ghasia na makundi pinzani ya waasi walivyochochea mzunguko wa ghasia hizo. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ukandamizaji unaofanywa na vikosi vya usalama na kundi la wapiganaji vijana la chama tawala la Imbonerakure, una lengo la kendelea kushikilia madaraka kwa nguvu na kwa kutumia njia zozote zile.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AP, AFP, Reuters
Mhariri: Daniel Gakuba

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com