1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watoto milioni mbili wa Yemen hawaendi shule, UN

John Juma
25 Septemba 2019

Shirika la UNICEF limesema masomo ya watoto wengine milioni 3.7 yako hatarini kwa sababu walimu hawajalipwa mishahara yao kwa zaidi ya miaka miwili.

https://p.dw.com/p/3QFfJ
Jemen humanitäre Lage Schule in Hodeidah
Picha: Reuters/A. Zeyad

Shirika la watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF limesema watoto milioni mbili hawaendi shule katika nchi ya Yemen iliyogubikwa na machafuko. Robo moja kati yao wamelazimika kuachana na masomo tangu machafuko yalipoanza kuongezeka Machi 2015.

Kwenye taarifa yao ambayo imetolewa leo, shirika la UNICEF limesema masomo ya watoto wengine milioni 3.7 yako hatarini kwa sababu walimu hawajalipwa mishahara yao kwa zaidi ya miaka miwili.

Sara Beysolow Nyanti ambaye ni mwakilishi wa UNICEF nchini Yemen amesema watoto wengi wanashindwa kuenda shuleni kufuatia machafuko, watu kukimbia makwao na mashambulizi katika shule.

Shirika hilo limeongeza kuwa kutokana na athari za moja kwa moja ya machafuko ambayo yameuvuruga mfumo dhaifu wa elimu katika taifa hilo maskini la Kiarabu, zaidi ya shule 2,500 nchini Yemen hazifanyi kazi.

Thuluthi mbili zimeharibiwa na mapigano, zaidi ya robo zimefungwa na nyingine zimegeuzwa kuwa kambi za kijeshi au za watu ambao makazi yao yameharibiwa na vita.

Watoto ambao wamepoteza makaazi kufuatia mashambulizi wanakabiliwa na changamoto za ukosefu wa shule za kusomea.
Watoto ambao wamepoteza makaazi kufuatia mashambulizi wanakabiliwa na changamoto za ukosefu wa shule za kusomea.Picha: Getty Images/AFP/E. Ahmed

Nyanti amesema watoto ambao hawaendi shule, wanakabiliwa na vitisho vya kila aina ikiwemo kulazimishwa kujiunga katika vita hivyo ambavyo vimedumu kwa miaka mitano sasa, kushirikishwa katika ajira japo wana umri mdogo na hata kujikuta katika ndoa ya mapema.

Nyanti ameongeza kwamba watoto hao wanapoteza fursa ya kukua katika mazingira ya kujaliwa na upendo ambapo mwishowe wanajikuta wamenaswa kwenye maisha magumu na ya uchochole.

Maelfu kwa maelfu ya watu haswa raia wameuawa tangu Saudi Arabia na washirika wake walipoingilia machafuko ya Yemen mnamo Machi mwaka 2015, kwa kuunga mkono serikali inayokumbwa na misukosuko, baada ya waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran kuudhibiti mji mkuu Sanaa.

Kufuatia vita hivyo, mamilioni ya watu wamepoteza makaazi na kuwaacha watu milioni 24.1 ambao ni zaidi ya theluthi mbili ya idadi jumla katika nchi hiyo wakihitaji misaada.

Miongoni mwa shule ambazo zimeharibiwa Yemn kufuatia mashambulizi
Miongoni mwa shule ambazo zimeharibiwa Yemn kufuatia mashambuliziPicha: DW/K. Al Banna

Kulingana na UNICEF, watoto milioni 1.8 walio na umri wa chini ya miaka mitano wanaugua maradhi ya utapiamlo uliopindukia.

Ijumaa iliyopita UNICEF ilisema zaidi ya watoto milioni 29 walizaliwa katika maeneo ya machafuko.

Shirika hilo liliongeza kuwa wazazi katika maeneo yanayokumbwa na vita, wanahitaji zaidi msaada pamoja na watoto wao ili waweze kukabiliana na masaibu yanayowakumba.

Umoja wa Mataifa umeelezea hali ya Yemen kuwa janga baya zaidi la kibinadamu.

Vyanzo: DPAE;