1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wataalamu wafichua mauaji ya kutisha Izium, Ukraine

19 Septemba 2022

Katika msitu kwenye eneo lililokombolewa hivi majuzi la Izium. Wataalamu wa kupima maiti wa Ukraine wanafukua miili iliyozikwa kwenye makaburi ya halaiki wakati wa ukaliaji kimabavu wa Urusi.

https://p.dw.com/p/4H2cX
Ukraine | Krieg | Massengräber in Izium
Picha: Emmanuelle Chaze/DW

Rais wa Ukraine Volodymir Zelensky ameapa mapambano yataendela kuyakomboa maeneo yaliyotekwa na Urusi huku Ukraine ikiripoti kuwa wanajeshi wake wamesonga mbele hadi katika ufukwe wa mashariki wa mto Oskil, na kutishia vikosi vya Urusi vinavyolikalia eneo la Donbas. Wakati hayo yakijiri, zaidi ya miili 400 inafukuliwa kutoka kwenye makaburi nje ya mji wa Izium.

Msitu kunakopatikana makaburi ya mji uko nje kidogo na mji wa Izium katika eneo la Ukraine la Kharkiv. Lakini kabla kuingia katika msitu huu, vilima vya mchanga vinaonekana chini ya miti, huku malori mawili makubwa yenye nambari 200 ikiwa imekolezwa kwa rangi upande wa ubavuni yakiwa yameezekwa kando ya barabara chafu. Namba hiyo katika lugha ya kijeshi ina maanisha maiti.

Wakati unapotembea kwenye njia za msitu huo ndivyo ukatili na unyama unavyodhihirika. Kila kilima cha mchanga ni kaburi. Ni eneo la kutisha ajabu, mazishi ya halaiki ya watu zaidi ya 400 waliokufa vifo vya kinyama kabisa chini ya udhibiti na ukaliaji kimabavu wa Urusi mashariki mwa Ukraine. Miili kadhaa tayari imeopolewa na kuhamishwa hadi katika chumba cha kuhifadhia maiti kwa uchunguzi zaidi. Lakini matokeo ya tathmini ya awali yanatisha. Maiti nyingi zinaonyesha dalili na mateso.

Watalaamu wa uchunguzi wa maiti wameomba msaada wa maafisa wa zima moto kufukua mabaki ya maiti za binadamu. Mmoja wa maafisa hao, Andreiy Vladimirovich Sergienko ameiambia DW kwamba, "Kazi yangu ni kufukua miili kabla wataalamu wa uchunguzi kubaini kilichotokea. Baadaye tunaziweka maiti kwenye mifuko na kuzisafirisha hadi katika vyumba vya kuhifadhia maiti. Hiki ni kipindi kigumu cha kutisha katika maisha yangu, na ni kwa mara ya kwanza kupitia uzoefu huu katika miaka yangu mitano ya kufanya kazi. Kisaikolojia nadhani tutahitaji msaada siku za usoni kwa sababu picha hizi zitakuwa katika fikra zetu milele."

Ukraine | Krieg | Massengräber in Izium
Makaburi yaliyotumiwa kufukia maiti kwa pamojaPicha: Emmanuelle Chaze/DW

Andreiy ameongeza kusema makaburi hayana majina isipokuwa nambari tu. Jumla ya watu 418 wamezikwa katika eneo hilo.

Hali ni ya kutisha

Kila upande kutoka mahala aliposimama Andreiy, makaburi mapya yanafukuliwa. Mwili unapofukuliwa wachimbaji na wataalamu wananyamaa kimya kwa muda kutoa heshima zao kwa maiti. Kutokana na idadi ya maiti zinazofukuliwa baadhi ya wataalamu wanatoa tathmini zao wakati huo huo, ambazo zinanakiliwa na maafisa wa polisi. Kunakuwa na kimya cha kutisha msituni kote. Sauti inayosikika ni ya nzi wanaofuata maiti, sauti za kamera zinazotumiwa kupigia picha na milio ya silaha, huku vita vikiendelea kuchacha kiasi mita mia moja mbali kidogo kutoka eneo hilo.

Mbele ya kundi ndogo la waandishi habari afisa aliyevalia nguo nyeupe za kujikinga anainama kwenye mwili ambao umetolewa. Analegeza nguo zake, akichakura kitu chochote kwenye mifuko kinachoweza kusaidia utambulisho wake. Baadaye anaendelea pole pole kuandika tathmini yake ya awali.

Alisema mwili ni wa mwanamume aliyekuwa na umri wa miaka 80. Mikono yake imefungwa nyuma, kichwa chake kimefunikwa na jaketi. Tezi zake dume zimepasuliwa, eneo la ndani la mapaja yake lina alama za mateso. Alipigwa na kitu kigumu kichwani kutokea nyuma, pengine na kitu chenye ncha kama kisu. Baadaye afisa huyo anavua glavu zake na anakaa kwenye gogo la mti ulioanguka, akikataa kusema lolote kuhusu ugunduzi wa kutisha aliouona.

Wengi waliouwawa ni wakazi wa Izium

Kwa mujibu wa mwendesha mashtaka ya uhalifu wa kivita wa Ukraine katika eneo la tukio, Volodymyr Lymar, watu wengi kati ya waliouwawa ni wakaazi wa eneo la Izium pamoja na wanajeshi baadhi. Akizungumza na DW Lymar alisema baadhi ya maiti zilitambuliwa lakini kwa kuwa vifo vyao vilitokea karibu miezi sita iliyopita, maiti nyingine ziko katika hali mbaya ya kuoza kiasi kwamba ni vigumu kufanya tamthmini yoyote.

Ukraine | Krieg | Massengräber in Izium
Baadhi ya maiti zilizofukuliwaPicha: Emmanuelle Chaze/DW

"Hii itahitaji uchunguzi wa ziada wa vinasaba, ikiwemo kulinganisha vinasaba na jamaa wa familia. Tunachoweza kukibaini hata hivyo ni dalili za vifo kutokana na matumizi ya nguvu. Baadhi ya maiti zinaonyesha dalili za uwezekano wa mateso."

Miongoni mwa maiti zilizopatikana zilikuwemo za wanajeshi 17 wa Ukraine katika kaburi la pamoja, mikono yao ikiwa imefungwa na dalili zikionyesha waliuliwa wakiwa karibu.

Emmanuelle Chaz, DW