1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wataalamu wa Silaha waanza kazi tena Syria

26 Septemba 2013

Wataalamu wa silaha wa Umoja wa Mataifa wamerudi katika maeneo ambako inadaiwa yalifanywa mashambulizi ya silaha za kemikali nchini Syria, huku wanadiplomasia wakikaribia muafaka juu ya azimio kwa ajili ya silaha hizo.

https://p.dw.com/p/19p1x
Msafara wa wataalamu wa silaha wa Umoja wa Mataifa wakielekea kazini
Msafara wa wataalamu wa silaha wa Umoja wa Mataifa wakielekea kaziniPicha: Reuters

Kwa mujibu wa mwandishi wa shirika la habari la AFP aliye katika mji mkuu wa Syria, Damascus, wataalamu hao wa silaha wa Umoja wa Mataifa wameondoka kwenye hotel yao, wakielekea katika eneo ambalo halikuweza kujulikana mara moja. Wataalamu hao waliwasili nchini Syria jana, na wanatarajiwa kukagua maeneo 14 ambako inadaiwa mashambulizi yalifanywa kwa kutumia silaha za kemikali.

Katika ujumbe wao wa awali, walichunguza mashambulizi ya tarehe 21 Agosti karibu na Damascus, ambamo inadaiwa silaha za kemikali zilitumika na kusababisha vifo vya mamia ya watu.

Hatua kuelekea azimio

Makubaliano yaliyofikiwa baada ya mashambulizi hayo kati ya Urusi na Marekani yalisitisha kitisho cha Marekani kuishambulia kijeshi Syria, katika kile ilichokiita kuiadhibu serikali ya nchi hiyo, kwa kutumia silaha za maangamizi zilizopigwa marufuku na Jumuiya ya kimataifa.

Makubaliano kati ya Urusi na Marekani yalinyamazisha milio ya ngoma za vita
Makubaliano kati ya Urusi na Marekani yalinyamazisha milio ya ngoma za vitaPicha: Reuters

Azimio la Umoja wa mataifa kuhusu makubaliano hayo, ambayo yanaitaka Syria kukabidhi silaha zake zote za kimekali ili ziteketezwe, linajadiliwa na mataifa makubwa duniani.

Akizungumza na kituo cha televisheni cha Telesur cha Venezuela, rais wa Syria Bashar al Assad amesema serikali yake itatimiza majukumu yake kulingana na makubaliano kati ya Marekani na Urusi.

Katika mahojiano hayo ambayo yalirushwa hewani jana, Assad alisema serikali yake itaheshimu makubaliano yote ambayo imeyatia sahihi. Alisema serikali yake tayari imeanza kutoa maelezo yanayohitajika kuhusu silaha zake za kemikali, kwa shirika la kimataifa la kudhibiti silaha hizo, OPCW. Rais Assad aliongeza kuwa wataalamu wa shirika hilo watawasili nchini Syria kuzikagua silaha hizo.

Bashar al Assad alisema haoni kikwazo chochote cha kuizuia serikali yake kutoa ushirikiano katika zoezi hilo, lakini alielezea wasiwasi, kwamba huenda wapinzani, ambao anawaita magaidi wanaweza kuwazuia wakaguzi hao kufika katika baadhi ya maeneo.

Inadaiwa kuwa mamia ya watu walikufa karibu na Damascus kutokana na shambulio la silaha za kemikali, Agosti 21.
Inadaiwa kuwa mamia ya watu walikufa karibu na Damascus kutokana na shambulio la silaha za kemikali, Agosti 21.Picha: Getty Images/Afp

Mataifa wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zimesema kuwa zimepiga hatua kujadili azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu silaha za kemikali za Syria, ambalo mwanadiplomasia mmoja wa kimarekani amesema litaluhusu matumizi ya nguvu za kijeshi dhidi ya Syria ikiwa itashindwa kulitekeleza.

Hata hivyo, Urusi ambayo ni mshirika wa serikali ya Rais Bashar al Assad inapinga azimio lolote linalojumuisha lugha ya matumizi ya nhguvu za kijeshi.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman