1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasoshalisti waondolewa madarakani Ureno

Bruce Amani
11 Machi 2024

Watawala wa kisoshalisti nchini Ureno wameondolewa madarakani baada ya miaka minane, huku chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Chega kikishuhudia uungwaji mkono ukiongezeka katika uchaguzi wa bunge.

https://p.dw.com/p/4dNMa
Waziri Mkuu wa Ureno Antonio Costa
Waziri Mkuu wa Ureno, Antonio Costa, akipiga kura yake kwenye uchaguzi wa bunge siku ya Jumapili (10 Machi 2024). Picha: Patricia de Melo Moreira/AFP/Getty Images

Chama cha siasa za wastani za mrengo wa kulia, Democratic Alliance, kilipata asilimia 29 ya kura na kukipiku kwa kura chache chama cha Kisoshalisti kinachofuata siasa za wastani za mrengo wa kushoto kilichopata asilimia 28.7.

Chama cha Chega, ambacho kina miaka mitano tangu kuasisiwa, kikiongozwa na mchambuzi wa kandanda kwenye televisheni, Andre Ventura, kimeimarika kutoka asilimia 7 ya kura katika mwaka wa 2022 hadi karibu asilimia 18 katika uchaguzi wa Jumapili..

Soma zaidi: Chama cha mrengo wa kulia huenda kikawatoa Wasoshalisti, Ureno

Chega itaongeza uwepo wake katika bunge lenye viti 230 mjini Lisbon kutoka 12 hadi 46, ambako Democratic Alliance itakuwa na viti 79 wakati Wasoshalisti wakiwa na 77.

Luis Montenegro, kiongozi wa chama cha Democratic Alliance, alitangaza ushindi, wakati mpinzani wake wa Kisoshalisti, Pedro Nuno Santos, akikiri kushindwa na kutangaza kuwa atahamia upinzani.