Wasiwasi watanda Gaza | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 17.05.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Wasiwasi watanda Gaza

Hali ya wasiwasi imetanda mjini Gaza kufuatia vifo vya watu watano hata baada ya makubaliano mapya ya kusitisha vita kufikiwa hapo jana.Mapigano makali kati ya makundi hasimu ya Hamas na Fatah yamekuwa yakiendelea kwa siku chache zilizopita jambo linalohofiwa kuvunja serikali ya umoja wa kitaifa iliyoundwa hivi karibuni.

Waandamanaji mjini Gaza

Waandamanaji mjini Gaza

Rais wa Palestina Mahmoud Abbas wa chama cha Fatah natarajiwa kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu Ismail Haniye wa Hamas yanayolenga kumaliza ghasia hizo.Wakati huohuo Israel inashikilia kuwa italipiza kisasi baada ya wapiganaji wa eneo la Gaza kurusha makombora nchini mwao na kujeruhi watu wane wiki hii.

Milio ya risasi ilisikika kote katika barabara mjini Gaza.Wapiganaji waliogubika nyuso zao na kujihami kwa silaha walizurura mjini wengine wakiwa kwenye mapaa ya nyumba.Hata hivyo makubaliano mapya ya kusitisha vita yanaonekana kudumu.

Makundi hayo mawili yanayohasimiana yalifanya makubaliano ya nne ya kusitisha vita katika kipindi cha siku chache ili kujaribu kumaliza ghasia zinazotishia serikali mpya ya kitaifa iliyoundwa miezi miwili iliyopita.

Katika kipindi cha saa chache baada ya makubaliano hayo kufikiwa,wafuasi wawili wa Fatah na wapiganaji watatu wa Hamas waliuawa katika visa viwili tofauti.Makundi hayo hasimu yalifikia makubaliano ya kusitisha vita mara tatu na kuvunjika baada ya saa chache kabla ghasia kuanza tena jumapili iliyopita. Umwagikaji damu huo umesababisha wakazi wa Gaza kujificha majumbani mwao huku wakikabiliwa na matatizo baada ya serikali ya Palestina kusitishiwa misaada ya fedha wakati chama cha Hamas kilipoingia madarakani mwaka jana.

Mapigano hayo aidha yanatishia juhudi za kufufua mpango wa amani unaosimamiwa na Jumuiya ya Milki za Kiarabu uliokwama kwa miaka sita.

Kwa upande mwingine Israel imeshambulia eneo la Gaza kwa makombora hapo jana na kusababisha vifo vya wapiganaji wanne.Shambulio hilo lilikuwa la kulipiza kisasi baada ya wapiganaji kuwashambulia.

Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert aliamuru hatua ya kulipiza kisasi baada ya kushambuliwa na wapiganaji wa Gaza.Mashambulio hayo yalianza baada ya mapigano kati ya Hamas na Fatah jumapili iliyopita na kusababisha vifo vya watu 43 wengi wao wafuasi wa Fatah.Zaidi ya watu 100 wamejeruhiwa katika ghasia hizo.

Makombora mengine mawili yalishambulia Israel hii leo moja likianguka kwenye shule iliyo mjini Sderot wa eneo la kusini.

Kulingana na tangazo la redio ya kijeshi ya Israel,jeshi lina orodha ya maeneo inayopanga kusahmbulia wakiwemo wanamgambon waliohusika na mashambulio hayo.Jeshi aidha huenda likashambulia makao ya wanamgambo hao mjini Gaza.

Hata hivyo jeshi hilo halina mpango wa kushambulia viongozi wa kisiasa wa chama cha Hamas.Wapiganaji wa chama hicho wamekiri kutekeleza mashambulio ya makombora katika kipindi cha siku tano zilizopita.

Tangu mapigano hayo kuanza siku ya Jumapili kati ya makundi hasimu,raia 4 wa Israel wamejeruhiwa na mashambulio ya makombora.Tangazo la Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert la kulipiza kisasi huenda likavunja makubaliano ya kusitisha yaliyofikiwa kati ya jeshi la Israel na wapiganaji.Makubaliano hayo yamedumu kwa miezi sita ingawaje bado ghasia zinatokea.Katika makubaliano yaliyofikiwa Novemba 26,Israel iliondoa majeshi yake katika Ukanda wa Gaza nao wapiganaji walipaswa kuacha kurusha makombora.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon,Umoja wa Ulaya vilevile Marekani wanatoa wito kwa ghasia hizo kumalizika huku mataifa ya Arabuni wakieleza wasiwasi wao hususan mustakabal wa Palestina.

Kwa mujibu wa msemaji wa Wizara ya Mambo ya nje ya Marekani Tom Casey ghasia hizo zinahatarisha hatua ya kutimiza ahadi ya dola milioni 60 ya Marekani kwa minajili ya kufadhili majeshi ya usalama yanayosimamiwa na Rais wa Palestina Mahmoud Abbas.

 • Tarehe 17.05.2007
 • Mwandishi Thelma Mwadzaya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CB45
 • Tarehe 17.05.2007
 • Mwandishi Thelma Mwadzaya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CB45
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com