1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wananchi wa Asia Kusini wasimama dhidi ya mateso ya Rohingya

1 Desemba 2016

Ni jambo gumu kwa mwanaadamu kujikuta nchi yake mwenyewe ya uzawa inamshinda kuikaa na hivyo kulazimika kuikimbia au kwa aliyekwishakuikimbia kushindwa kurejea pindi anapotaka kufanya hivyo, lakini ni gumu zaidi pale anapojikuta hana kabisa hata hiyo nchi anayoweza kuiita yake kwa kuwa tu wenye mamlaka wameamualia kuwa yeye si raia wa mahala popote pale kwenye ardhi hii ya Mungu Muumba.

https://p.dw.com/p/2Tams

Jamii ya Rohingya ni Waislamu wenye asili ya Indo-Aryan kutoka jimbo la Rakhine, hivi sasa sehemu ya Myanmar. Wenyewe wanaamini kuwa ndio wakaazi asili wa jimbo hilo, ingawa kuna wanahistoria wanaodai kuwa ni wahamiaji kutoka Bengali tangu zama za utawala wa Muingereza kwenye mataifa hayo ya kusini mwa Asia.

Baada ya uhuru wa Myanmar mwaka 1948 na kisha Vita vya Ukombozi vya Bangladesh vya mwaka 1971, jamii hii imekuwa ikielezewa kama moja kati ya watu wanaoteseka sana duniani, wakiwa hawana hata serikali moja inayowatambua kuwa raia wake.

Maelfu ya watu kwenye mataifa ya Malaysia, Indonesia na Myanmar waliamua kuuvunja ukimya wao juu ya jaala ya jamii ya Rohingya, na kwa mara ya kwanza wakaingia mitaani kwa pamoja mwishoni mwa mwezi Novemba, kuzitaka serikali zao zisake suluhisho la kudumu kwa jamii  hiyo.

"Matakwa yetu kwa hakika ni kwamba serikali ya Myanmar inapaswa kuwalinda watu wa Rohingya haraka sana, wasingojee Umoja wa Mataifa au yeyote mwengine kuingilia. Naye kiongozi wa Myanmar, Aung San Suu Kyi, awalinde watu walio wachache kama ambavyo humu nchini mwetu wachache wanalindwa na serikali. Aige mfano kwa kuilinda asilimia 10 ya Rohingya walioko nchini mwake", alisema mkuu wa Muungano wa Mashirika ya Kiislamu nchini Malaysia, Amir Hamzah, aambaye aliongoza maandamano hayo mjini Kuala Lumpur. 

Ni kijembe cha hali ya juu kwamba jina la mpigania demokrasia na haki za binaadamu, na ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel, Aung San Suu Kyi, linatajwa katika upande mchafu wa kadhia hii - yaani upande wa ukandamizwaji wa jamii ya Rohingya. 

Mwanamke huyu jasiri na ambaye mwenyewe aliwahi kusema kuwa hata mateso dhidi ya mtu mmoja ni mengi, amejikuta amewekwa katikati ya suala hili: upande mmoja ni jamii kubwa ya Buddha, jamii yake, na ambayo ndiyo iliyosimama naye muda wote wa mapambano ya kudai haki za kidemokrasia kutoka utawala wa kijeshi, na upande mwengine ni matakwa ya kibinaadamu ya kuwahurumia na kuwatendea haki wale wanaonyimwa haki hizo - jamii ya Rohingya ambao ni Waislamu.

Katika ziara yake ya karibuni mjini Tokyo, Japan, mwanasiasa huyo alionekana kulifunika suala la Warohingya kwenye kapu la jumla jamala.

Rohingya Flüchtlinge Myanmar Bangladesch
Wakimbizi wa Rohingya wakilia baada ya kukamatwa na walinzi wa mpakani wa Bangladesh kwa tuhuma za kuvuuka mpaka kinyume cha sheria.Picha: Reuters/M.P.Hossain

"Daima nimekuwa nikipinga ghasia, hasa kwenye siasa, na ninasikitika kwamba watu wetu hawajaweza kutatua tafauti zao kwa kuzungumza na sio kwa fujo. Ama kwenye suala la ikiwa Rohingya ni raia au la, hilo linategemeana zaidi na ikiwa wanatimiza vigezo vya uraia kama vinavyoelezwa sasa na sheria zilizopo", aliwaambia waandishi wa habari.

Urithi mbaya wa siasa za kijeshi kuelekea Rohingya

Lakini hicho anachokizungumzia Aung Saan Suu Kyi kuwa sheria ya uraia, ni ile ya mwaka 1982, iliyowekwa na serikali ya kijeshi ya Jenerali Ne Win, ambayo iliwapiga marufuku watu wa jamii ya Rohingya, kuwa raia wa nchi hiyo. 

Utawala wa kijeshi ambao uliitawala Myanmar kwa nusu karne nzima ulitegemea sana kulichanganya suala la uraia wa nchi hico na uumini wa dini ya Kibuddha hasa wa madhehebu ya Theravada, na hivyo kwa makusudi kabisa kuwatenga Waislamu wa jamii ya Rohingya na hata raia wenye asili ya China kama vile jamii za Kokangs na Panthays. 

Hata kwenye mapambano ya kudai demokrasia kutoka utawala huo wa kijeshi, baadhi ya wanaharakati hawakuwa wakiwachukulia Rohingya kuwa ni wazalendo wa nchi. Inahofiwa na wengi kuwa tabia hii ya utawala wa kijeshi kuelekea Rohingya imerithiwa na utawala wa kiraia chini Aung Saan Suu Kyi.

"Hili ni eneo ambalo wanaishi Mabuddha na Waislamu wengi, lakini serikali ya Myanmar inachochea machafuko. Inayahamishia matatizo yake kwa mataifa jirani. Warohingya wengi pia wanaishi Indonesia, Thailand na Malaysia. Hivyo ni jukumu la Myanmar kuwalinda wanaoishi ndani yake, sio jukumu la nchi zilizobakia hapa. Ndio maana lazima Mnyanmar ibebe dhamana na kuwarejeshea Warohingya uraia wao haraka iwezekanavyo", anasema Mohammed Noor, kiongozi wa jamii ya Rohingya nchini Indonesia, akiongeza kuwa Myanmar mpya haipaswi kabisa kufuata siasa ya kidikteta kuelekea raia wake wenyewe.

Ila hilo la kurejeshewa uraia linaonekana kuwa mbali sana na kuwa. Kinyume chake, kwa mujibu wa shirika la haki za binaadamu la Human Rights Watch, serikali ya Myanmar - ambayo iko chini ya Saan Suu Kyi, inahusika na kampeni ya kuwaangamiza watu hao wa jamii ya Rohingya kwenye jimbo la Rakhine.

Mashambulizi ya Myanmar dhidi ya Rohingya

Indonesien Jakarta Protest vor Botschaft von Myanmar
Maandamano mbele ya ubalozi wa Mnyanmar mjini Jakarta, Indonesia, yalimzuwia Aung Saan Suu Kyi kuitembelea nchi hiyo.Picha: picture-alliance/dpa/B. Indahono

Picha za satalaiti zilizotolewa na Human Rights Watch mnamo mwezi Novemba, zinaonesha kuharibiwa vibaya kwa vijiji vinavyokaliwa na watu wa jamii Rohingya kwa moto.

Nyumba 430 zilionekana kwenye picha zilizochukuliwa tarehe 22 Oktoba, 3 na 4 Novemba mwaka huu wa 2016, zikiwa zimeteketea kwa moto, zote kwenye wilaya ya Maundaw. Na bado, linasema shirika la Human Rights Watch, huenda idadi kamili ya nyumba zilizoteketezwa moto ni kubwa zaidi.

Ni ugunduzi huu wa Human Rights Watch uliosababisha maandamano katika miji kadhaa ya kusini mwa Asia na pia wito wa kimataifa wa kutaka uchunguzi huru, na ni maandamano yaliyomfanya Aung Saan Suu Kyi kufuta ziara yake ya Indonesia. Lakini kwa upande mwengine, jibu la serikali ya Mnyamar kwa ripoti ya Human Rights Watch likawa kwanza ni kuwapiga marufuku waandishi wa habari kukaribia eneo lililorikodiwa tukio lenyewe, na kisha kukanusha kabisa kutokea kwake, ikiwatupia lawama Warohingya wenyewe kuwa wahusika wakuu wa njama hii.

"Tunapoangalia matukio haya huko nyuma na ya miaka mitanok iliyopita, mambo kama haya yalitokea, yaani nyumba kuchomwa. Tulikuwa na ushahidi kuwa hii ni tabia ya watu wa Rohingya. Ndicho wanachokifanya. Kwa kufanya hivi, huwa wanapata msaada wa kibinaadamu na ujenzi mpya wa nyumba zao au kuhamishiwa maeneo  mengine. Tunaweza kusema hapa leo kwenye mkutano huu na waandishi wa habari, kuwa wamekuwa wakifanya hivyo." Msemaji wa Ofisi ya Rais wa Myanmar, Zaw Htay, aliwaambia waandishi wa habari mjini Yangoon.

Rohingya wateseka pia nje ya Myanmar

Ripoti zinaonesha kuwa ukandamizaji wa dola dhidi ya Warohingya yamepamba moto katika siku za hivi karibuni nchini Myanmar, baada ya mashambulizi yaliyokuwa yakidaiwa kufanywa na wanamgambo wa Kiislamu dhidi ya vituo vya polisi. Ambapo hata katika hali ya amani, jamii hii imekuwa ikijikuta ikinyimwa huduma za afya, elimu, na nyengine za kimsingi kutokana na kukataliwa kuwa raia, katika wakati wa machafuko kama hivi hali huzidi kuwa mbaya. Mauaji, uteswaji, ubakwaji, na kufukuzwa kwenye makaazi yao, ndio jaala ya jamii hii kwa miaka nenda miaka rudi sasa.

Rohingya Flüchtlinge Myanmar Bangladesch
Wakimbizi wa jamii ya Rohingya wakiwa kwenye kampi ya wakimbizi ya Kutupalang nchini Bangladesh.Picha: Reuters/M.P.Hossain

Lakini, watu wa jamii ya Rohingya hawateseki nchini Myanmar pekee, nchi wanayoichukulia kuwa ndiyo yao ya asili. Wanateseka pia wanapoyakimbia makaazi yao kukimbilia mataifa jirani ya Bangladesh, Indonesia na Thailand, ambako kwa hakika nako wanakataliwa. Kwa mfano, mwishoni mwa mwezi Novemba, Bangladesh ilizirejesha boti kadhaa zilizobeba wanawake na watoto wa Kirohingya wanaokimbia mauaji na mateso Myanmar. 

Shirika la habari la AFP liliripoti kushuhudia angalau boti nane kwenye Mto Naf unaolitenganisha jimbo la Rakhine la Myanmar na mkoa wa kusini wa Bangladesh zikirejeshwa na walinzi wa Bangladesh, licha ya kwamba mjini Dhaka, waandamanaji walikuwa wamejaa mitaani kuilaani Myanmar kwa kuwashambulia ndugu zao hao.

"Lazima kianzishwe kikosi cha kulinda amani chini ya Umoja wa Mataifa ili Waislamu hawa wa Mnyamnar waweze utu wao. Tumepata habari kuwa wengi wao wako kwenye hali mbaya sana na wanaelea kwenye Mto Naaf. Hawa lazima wapewe hifadhi hapa Bangladesh kadiri inavyowezekana." Mufti Sakhawat Hossain wa jumuiya ya Hefezat-e-Islam, aliyekuwa miongoni mwa waandamanaji hao, anadhani kunalazimika kuwepo hasa uingiliaji kati wa kimataifa.

Lakini si wito wa kimataifa wala wa waandamanaji hawa unaoingia kwenye sikio la serikali ya Bangladesh.

Badala ya kuwapokea maelfu ya Warohingya hao wanaokimbia kunajisiwa, kuuawa na kuteswa, serikali ya Sheikh Haseena mjini Dhaka ilituma ujumbe mkali kwa serikali ya Myanmar kuwa iwazuwie watu wasitoroke. 

Ni kweli kuwa Bangladesh inawahifadhi Warohingya wapatao 500,000, lakini kati yao ni 30,000 tu ambao hadi sasa imewatambua kuwa wakimbizi na kuwasajili rasmi, huku wakiwalazimisha wakae kwenye makambi machafu na dhaifu, yasiyo huduma wala usalama.

Waliobakia wanazururazurura na kila siku wakiwa hatarini kukamatwa na kupakiwa kwenye maboti kuvuushwa kurejeshwa Rakhine, kwenye mateso yale yale ya siku nenda siku rudi. 

Umma wa watu wa kawaida, ambao umechoshwa na mateso wanayowapata wanaadamu wenzao, ndio ulioinuka kwenye mataifa ya kusini mwa Asia hivi sasa, kuzidai serikali zao kuchukuwa hatua za haraka kuwanusuru maelfu ya watu wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar.

Ni shinikizo hili ambalo lilimfanya hata Aung Saan Suu Kyi kufuta ziara yake ya Jakarta, Indonesia, akihofia maandamano ya umma dhidi yake. Ndio pia ulilolifanya baraza la mawaziri la Malaysia kutoa tamko rasmi na kali dhidi ya mwanachama mwenzao wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Asia Kusini (ASEAN). Ni sauti za wanyonge kwa ajili ya wanyonge wenzao zilizoyawezesha haya. Na yumkini, huko tuendako zikaibadilisha jaala ya Rohingya milele.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters/AP
Mhariri: Saumu Yussuf