1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi Nigeria wafyatua risasi dhidi ya waandamanaji

Yusra Buwayhid
21 Oktoba 2020

Watu wawili wamejeruhiwa hapo jana mjini Lagos, Nigeria, baada ya wanajeshi kuwafyatulia risasi za moto waandamanaji wanaopinga ukatili wa polisi, kulingana na mashuhuda.

https://p.dw.com/p/3kDK8
Nigeria Abuja | End Sars Proteste | Demonstranten
Picha: Kola Sulaimon/AFP/Getty Images

Taarifa hizo ni kulingana na mashuhuda wanne waliozungumza na shirika la habari la Reuters. Jeshi la Nigeria hata hivyo limedai kuwa wanajeshi wake hawakuweko katika eneo hilo la maandamano JUmanne. Serikali imesema itafanya uchunguzi dhidi ya tukio hilo.

Aidha Jumanne kumetangazwa amri ya kutotembea usiku ya muda wa masaa 24 katika mji wa Lagos ambao ni kitovu cha biashara Nigeria, wakati vurugu zikiongezeka katika maandamano ambayo yametikisa miji kadhaa nchini humo.

Ni moja ya majimbo matatu kati ya 36 ya Nigeria yaliyotangaza hatua kama hiyo katika siku mbili zilizopita. Mkuu wa polisi wa kitaifa pia aliamuru kupelekwa mara moja kwa vikosi vya kupambana na ghasia kote nchini kufuatia kuongezeka kwa mashambulio kwenye vituo vya polisi, kulingana na msemaji wa polisi.

Shirika la kutetea haki za binadamu Amnesty International limesema lina ushahidi wa matumizi mabaya ya nguvu na kusababisha vifo vya waandamanaji, na kwamba takriban watu 15 wameuawa tangu maandamano hayo kuanza.

Malalamiko dhidi ya SARS yamekuweko kwa miaka mingi

Nigeria Lagos | Protest gegen Polizeigewalt
Mwandamanaji akiwa amesimama juu ya gari akipinga ukatili wa polisi lagos, Nigeria.Picha: Seun Sanni/Reuters

Rais Muhammadu Buhari Jumanne alifanya mazungumzo na waziri wa ulinzi na mkuu wa vikosi vya ulinzi kujadili usalama wa kitaifa, kulingana na maafisa wawili kutoka ofisi ya rais, wakizungumza na shirika la habari la Reuters kwa sharti la kutotajwa majina.

Msemaji wa rais hakupatikana kutoa maoni yake juu ya madai hayo ya utumiaji wa risasi dhidi ya waandamanaji.

Kwa zaidi ya wiki mbili, maelfu ya raia wa Nigeria wamekuwa wakiandamana kote nchini humo dhidi ya ukatili unaofanywa na Kikosi Maalum cha Kupambana na Ujambazi (SARS).

Maandamano hayo yalizuka baada ya na video kuanza kusambaa mitandaoni mwanzoni mwa mweziOktoba inayowaonyesha maafisa wa SARS wakimpiga risasi mtu mmoja kusini mwa jimbo la Delta. Polisi walikana kuhusika na tukio hilo la kutumia risasi.

Kwa miaka mingi makundi ya kutetea haki za binadamu yamekuwa yakikishutumu kikosi hicho kwa unyanyasaji, mateso na mauaji ya raia.

Vyanzo: (dpa,rtre)