1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanaharakati wa mazingira waitwisha DR Congo mzigo wa lawama

Zainab Aziz Mhariri: Grace Patricia Kabogo
6 Machi 2020

Wanaharakati wa mazingira wa shirika lisilo la kiserikali la Greenpeace wameilaumu serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa kuidhinisha mikataba mipya ya ukataji miti katika msitu mkubwa wa Bonde la Congo.

https://p.dw.com/p/3YyhJ
Brasilien Symbolbild illegale Brandtrodung
Picha: AFP/R. Alves

Msitu huo ni mmoja kati ya sehemu kuu za misitu asilia duniani yenye uwezo wa kukabiliana na ongezeko la joto. Wanaharakati wa Greenpeace wamedai kuwa waziri wa Mazingira wa Congo, Claude Nyamugabo alisaini mikataba tisa mnamo mwezi Januari mwaka huu. Kulingana na wanaharakati hao, hayo yametokea wiki chache baada ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kupewa dola milioni 12 za misaada ya kimataifa kama sehemu ya mpango wa usimamizi endelevu wa misitu nchini humo.

Akijibu tuhuma hizo waziri Nyamugabo aliliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP, pembezoni mwa mkutano wa sera ya misitu katika mji mkuu Kinshasa siku ya Jumatano kwamba hakuna mikataba mipya iliyotiwa saini isipokuwa kilichotokea ni kwamba jina moja kati ya kampuni zilizopewa kandarasi ya ukataji miti limebadilika. Msitu wa Bonde la Congo, ni wa pili kwa ukubwa ulimwenguni baada ya msitu wa Amazon uliopo Amerika ya Kusini.

Msitu wa Amazon
Msitu wa AmazonPicha: picture-alliance/dpa/A. C. Araujo

Wakati huo huo, shirika la Greenpeace limeilaumu pia serikali ya Bulgaria kwa kuruhusu uchomaji taka kwa kiwango kikubwa. Mwanaharakati wa mazingira wa Bulgaria, Meglena Antonova amesema hatua ya wizara ya mazingira ya nchini mwake sio halali. Antonova amesema uchomaji taka kwa wingi ni lazima upitishwe baada ya majadiliano na umma. 

Wanaharakati wa mazingira nchini Bulgaria pamoja na mwakili wao wanailaumu serikali kwa kukiuka taratibu za kupitishwa idhini na kuwaweka Wabulgaria gizani juu ya hatari za kiafya na mazingira kutokana na kuchoma taka katika vinu vya zamani. Wanaoendesha kinu cha Bobov Dol walipata idhini ya kuchoma taka Aprili 2019.

Kulingana na Shirika la Kimataifa la Utafiti wa Saratani, linaloainisha uchafuzi wa hewa kwa jumla, Bulgaria ni kati ya nchi za Ulaya zilizo na kiwango cha juu cha PM 2.5, yaani mchanganyiko wa chembe chembe ndogo za vumbi, uchafu na moshi zilizo hewani ambazo viwango vyake vikizidi husababisha uchafuzi wa hewa na pia husababisha athari za kiafya. Bulgaria pia ni kati ya nchi za Ulaya yenye viwango vya juu zaidi vya carbon monoxide na sulfur dioxide.

Vyanzo: AFP/RTRE