1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Janga

Wakimbizi wapitia maeneo hatarishi kutoroka vita Kordofan

30 Desemba 2025

Maelfu ya raia wa Sudan wanaendelea kukimbia makazi yao kufuatia mapigano makali yanayoendelea katika jimbo la Kordofan, ambalo sasa limegeuka kuwa uwanja mpya na hatari zaidi wa vita vya zaidi ya miezi thelathini kati.

https://p.dw.com/p/568b5
Tschad | Sudanesische Flüchtlinge bei Lebensmittelverteilung in Adré
Picha: Nicolo Filippo Rosso/UNHCR

Wengi wa wakimbizi hawa wanalazimika kutembea kwa wiki kadhaa kupitia maeneo hatarishi, huku njaa, hofu na ukosefu wa msaada vikiendelea kuongezeka.

Kwa siku nane mfululizo, mkulima wa Sudan, Ibrahim Hussein, aliiongoza familia yake kupitia milima na mabonde hatarishi akijaribu kuokoa maisha yao. Walikuwa wanakimbia mapigano makali katika eneo la kusini mwa Kordofan, karibu na mpaka wa Sudan Kusini. "Tulikiacha kila kitu,” anasema Hussein mwenye umri wa miaka 47. "Mifugo yetu, mazao ambayo hatukuyavuna, yote tumeyaacha.”

Hussein alizungumza akiwa mjini Kosti, katika jimbo la White Nile, takriban kilomita 300 kusini mwa mji mkuu Khartoum. Mji huu unaodhibitiwa na jeshi umegeuka kuwa hifadhi ya mamia ya familia zinazokimbia vurugu Kordofan, eneo lenye utajiri mkubwa wa mafuta.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, karibu watu elfu hamsini na tatu wamelazimika kuyahama makazi yao katika wiki za hivi karibuni, baada ya wanamgambo wa RSF kuimarisha mashambulizi yao kufuatia kuteka ngome ya mwisho ya jeshi katika eneo la Darfur mwezi Oktoba. Tangu wakati huo, RSF imechukua udhibiti wa Kordofan Magharibi na kuitwaa Heglig, eneo lililopo juu ya shamba kubwa zaidi la mafuta nchini Sudan.

Sudan: Suluhisho la kisiasa haliwezi kupatikana bila vita kusitishwa

Wakati mapigano yakiendelea na juhudi za kimataifa za upatanishi zikiendelea kujadiliwa, uongozi wa jeshi la Sudan unasema suluhisho la kisiasa haliwezi kupatikana bila kusitishwa kwanza kwa mapigano.

Sudan |  Abdel Fattah al-Burhan
Abdel Fattah al-Burhan, Mkuu wa Jeshi la Sudan.Picha: AFP

"Baada ya mapigano kumalizika na silaha kuwekwa chini, ndipo tunaweza kuingia katika hatua inayofuata. Lakini kuchanganya suluhisho la kijeshi na la kisiasa wakati operesheni za kijeshi zinaendelea, sidhani kama amani inaweza kupatikana. Ndiyo maana tunaiambia tena Marekani na Rais Trump kwamba kama kweli anataka kuwa mtu wa amani mwaka huu, ni lazima aangalie suala la Sudan kwa mtazamo wa wananchi wa Sudan,”alisema Abdel Fattah al-Burhan, Mkuu wa Jeshi la Sudan.

Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji, IOM, karibu watu elfu nne waliwasili Kosti ndani ya siku mbili pekee wiki iliyopita, wakiwa na njaa, hofu na uchovu mkubwa. Wengi wao ni wanawake na watoto, huku wanaume wachache wakisalia nyuma kwa hofu ya kuuawa au kutekwa nyara.

Mashirika ya misaada yanasema barabara kuu si salama tena, na familia zinalazimika kutumia njia ndefu zisizo na uhakika, mara nyingi wakilala porini. Safari ambazo hapo awali zilichukua saa nne, sasa zinawalazimu watu kutembea kwa siku kumi na tano hadi thelathini kupitia maeneo yaliyojaa mabomu ya ardhini. Katika mwezi huu pekee, mashambulizi ya droni yaliripotiwa kulenga shule ya chekechea na hospitali katika mji wa Kalogi, kusini mwa Kordofan, na kuua watu zaidi ya mia moja, wakiwemo watoto sitini na watatu.

Wakimbizi wanaishi katika mazingira mabaya

Wakimbizi wengi sasa wanaishi katika shule na majengo ya muda yaliyojaa kupita kiasi. Adam Eissa, mkulima mwingine mwenye umri wa miaka 53, anasema alilazimika kutumia dola mia nne kuwaokoa mkewe, watoto wake wanne na mama yake mzee. Wengine wasiokuwa na uwezo huo hawana chaguo—wanabaki au wanatembea kwa miguu.

Wakati huohuo, miji kama Kadugli na Dilling inayodhibitiwa na jeshi bado imezingirwa, huku mamia ya maelfu wakikabiliwa na hatari ya njaa kali. Umoja wa Mataifa unaonya kuwa iwapo mapigano hayatasitishwa, kuna hatari ya kurudiwa kwa mauaji na uhalifu mkubwa wa kivita kama ulioshuhudiwa awali Darfur.

Kwa wakazi wengi wa Kordofan, uchaguzi unabaki kuwa mgumu—kukimbia kwa gharama kubwa na hatari, au kubaki wakikabili njaa, magonjwa na mashambulizi ya kila siku.

Suluhisho la mzozo wa Sudan liko wapi?