Wageni wamiminika Brazil, wenyeji waondoka | IDHAA YA KISWAHILI | DW | 24.06.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

IDHAA YA KISWAHILI

Wageni wamiminika Brazil, wenyeji waondoka

Wakati mashabiki wa kandanda kutoka sehemu mbalimbali duniani wakiwasili Brazil kushuhudia fainali za kombe la dunia zinazoendelea nchini humo, nao raia wa nchi hiyo wanapanda ndege na kuondoka

Wanaenda kuishi katika nchi za jirani sababu ikiwa ni kupanda kwa gharama za maisha pamoja na makelele ya mashabiki wa soka. Ni ngumu kuamini kuwa raia wengi wa Brazil ambao wanajulikana kuwa ni wapenzi wakubwa wa mchezo wa mpira wa miguu hivi sasa inawabidi waikimbie nchi yao kwa muda na kupisha raia wa nchi nyingine ambao wamekuja kushuhudia michuano ya kandanda ya kombe la dunia inayoendelea nchini humo.

Kwa mujibu wa shirika linalohughulika na masuala ya usafiri nchini Brazil, tokea mwaka huu uanze, zaidi ya asilimia 20 ya raia wa nchi hiyo wamesafiri kwenda nje ya nchi na kufanya kiwango hicho kuwa ni kikubwa ukilinganisha na kile cha mwaka jana cha mwezi juni na julai

WM 2014 Gruppe F 2. Spieltag Argentinien Iran

Mashabiki wa kandanda wakitazama mechi ya Kombe la Dunia katika fukwe za Copa Cabana, nchini Brazil

Lakini inaelezwa kuwa badhi ya raia wanakwenda kuishi nje ya nchi yao katika kipindi hiki cha fainali za kombe la dunia ikiwa ni njia ya kujiongezea kipato zaidi kwa kukodisha makazi yao kwa mashabiki wa soka kutoka nje ya Brazil ambapo hadi sasa idadi yao imefikia laki sita.

Mmoja kati ya nyota wa kandanda Brazil na dunia nzima, Ronaldinho Gaucho nae imembidi ahame katika nyumba yake ili aikodishe katika kipindi hiki cha michuano ya kombe la dunia kwa nia ya kujipatia fedha zaidi, Gaucho anaipangisha nyumba yake hiyo kwa dola15, 462 lakini bei hiyo imekuwa ikielezwa kuwa ni kubwa sana licha ya yeye mwenyewe kuitetea kupitia katika mtandao wake wa Twitter kuwa nyumba yake inakila kitu cha kifahari.

Kwa upande mwingine, kitendo cha raia wengi wa Brazil kwenda kuishi nchi za jirani kimeathiri utalii wa ndani wa nchi hiyo kwani idadi ya raia ambao wanasafiri kuelekea katika miji mbalimbali ya Brazil imepungua kwa kiasi kikubwa.

Kumekuwepo na kundi la raia wengi wa Brazil ambao wamekuwa wakipinga vikali nchi yao kuandaa michuano hiyo ya kombe la dunia wakati ambapo nchi yao bado inakabiliwa na changamoto nyingi katika huduma za jamiii lakini serikali ya nchi hiyo imeendelea kusisitiza kuwa michuano hiyo itasaidia kukuza uchumi wa Brazil.

Mwandishi: Anuary Mkama/DW
Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com