1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafungwa 12 wafa kutokana na kipindupindu Kamituga

Saumu Mwasimba
22 Desemba 2022

Wafungwa 12 wamefariki dunia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya kuugua ugonjwa wa kipindupindu ndani ya gereza kuu la mji wenye madini mengi wa Kamituga katika mkoa wa Kivu Kusini.

https://p.dw.com/p/4LK7k
Mosambik Klinik in Metuge
Picha: Adrian Kriesch/DW

Mbali na waliofariki, hospitali ya Kamituga imewapokea wafungwa wengine 31 walioambukizwa ugonjwa huo kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema licha ya hali hiyo ya magonjwa inayoendelea, wafungwa wanaendelea pia kukosa chakula, hali ambayo inaweza kudhoofisha afya zao zaidi.

Waziri wa Afya katika jimbo la Kivu Kusini Masine Kinenwa amesema kwa sasa juhudi zinafanyika ili kudhibiti kipindupindu kwenye eneo hilo.

Kinenwa amesema kuna ujumbe wa madaktari toka idara ya afya umeelekea Kamituga ukiambatana na madaktari wasiokuwa na mipaka MSF, maafisa wa Shirika la Afya Duniani, WHO, pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia Watoto, UNICEF, katika juhudi za kujaribu kuudhibiti ugonjwa huo.