Wafadhili waipatia Mali zaidi ya dala milioni 455 | Matukio ya Kisiasa | DW | 29.01.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Wafadhili waipatia Mali zaidi ya dala milioni 455

Maduka yanayomilikiwa na "waarabu" wanaoshirikiana na wafuasi wa itikadi kali yameporwa mjini Timbuktu katika wakati ambapo wafadhili mjini Addis Abeba wameiahidi Mali msaada wa kijeji na kiutu

Wanajeshi wa Ufaransa na wale wa Mali wanaulinda uwanja wa ndege wa Timbuktu

Wanajeshi wa Ufaransa na wale wa Mali wanaulinda uwanja wa ndege wa Timbuktu

Mamia ya watu wamevunja maduka wanayofikiri yanayomilikiwa na watu kutoka Algeria,na Mauritania wanaotuhumiwa kuwaunga mkono wafuasi wa itikadi kali wanaoshirikiana na mtandao wa kigaidi wa Al Qaida huko Timbuktu.Watu hao wamebeba kila walichokiona,kuanzia televisheni hadi kufikia vyakula na vyombo vya majumbani.Kwa mujibu wa maripota wa shirika la habari la Ufaransa AFP silaha pia zimegunduliwa katika baadhi ya maduka hayo.

Wanajeshi wa Mali hawajakawia kuingilia kati kuzuwia visa vya kupora mali.

Hapo awali shirika linalopigania haki za binaadam Human Rights Watch liliwatolea mwito viongozi wa Mali wachukue hatua zinazohitajika kuwahami wananchi na visa vya kulipiza kisasi.Shirika hilo limezungumzia kitisho cha kuzuka mivutano ya kikabila katika eneo la kaskazini ambako uhasama ni mkubwa kati ya jamii ya watu wenye asili ya kiarabu na ile ya watu weusi ambao ndio walio wengi nchini Mali.

Wafadhili waahidi msaada wav kijeshi na kiutu

Mali Geberkonferenz in Addis Abeba 29.01.2013

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Laurent Fabius akihutubia mkutano wa wafadhili mjini Addis Abeba

Wakati huo huo mjini Addis Abeba nchini Ethiopia,wawakilishi wa Umoja wa Afrika,Umoja wa ulaya,Japan,Marekani na Umoja wa Mataifa wakihudhuria mkutano wa wafadhili ,wamekubali kuipatia Mali msaada wenye thamani ya dala milioni 455.53 kukidhi mahitaji ya kijeshi na kiutu.

"Hali inahitaji jibu thabiti na la haraka la kimataifa,kwasababu inatishia usalama wa Mali,eneo,bara na hata zaidi ya hapo" amesema mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika,bibi Nkosazana Dlamini Zuma.

Matamshi kama hayo yametolewa pia na rais Boni Yayi wa Benin aliposema:"Ni suala linalolihusu eneo lote la Sahel na Sahara.Kwasababu ni suala la kupatikana amani na utulivu.Tunataka kusisitiza,tunahitaji amani na utulivu ili kuwa na mustakbal mwema.

Wakati huo huo wanajeshi 3500 wa Ufaransa na 1900 wa kiafrika wakiwemo wa Tchad na Niger wanaakutikana nchini Mali wakisaidiana na wanajeshi wa nchi hiyo.

Rais wa mpito aahidi uchaguzi haraka

Dioncounda Traore

Rais wa mpito wa Mali Dioncounda Traore

Mjini Timbuktu,kuna uhaba wa chakula na ukosefu wa,umeme,maji na mawasiliano ya simu yaliyokatwa na waasi kabla ya kukimbia .

Rais wa mpito wa Mali Dioncounda Traoré amesema mjini Addis Ababa anataraji kuitisha uchaguzi haraka iwezekanavyo nchini mwake.Hilo ni mojawapo ya masharti yaliyotolewa na wafadhili katika mkutano wao mjini humo hii leo.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com