Wabunge wa Uingereza wapiga kura kuchelewesha uamuzi wa mpango wa Brexit | Matukio ya Kisiasa | DW | 19.10.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Wabunge wa Uingereza wapiga kura kuchelewesha uamuzi wa mpango wa Brexit

Wabunge Uingereza wamepiga kura ya kuchelewesha kuuyafanyia uamuzi mpango wa Brexit wa Waziri Mkuu Boris Johnson wa kujiondoa katika Umoja wa Ulaya. Wamedai wanahitaji muda zaidi kuyaelewa yaliyomo kwenye mpango huo.

 Wabunge waliamua kwa kura 322 dhidi ya 306 kuunga mkono hatua iliyowasilishwa bungeni na mbunge wa muda mrefu Oliver Letwin. Wabunge hao wamedai kwamba wanahitaji muda zaidi kuyaelewa vizuri yaliyomo kwenye mpango huo kabla ya tarehe ya mwisho ya Oktoba 31. 

Matokeo hayo yanaahirisha hatua ya kuupigia kura mpango wa Brexit, hadi pale sheria zote zinazoambatana na mpango huo kupitishwa bungeni.  Aidha Johnson analazimika kuomba aongezewe muda kutoka Umoja wa Ulaya ili kuiepusha nchi hiyo kujitoa Oktoba 31 bila ya mpango wowote.

Johnson ameyakataa matokeo hayo, licha ya kukiri kwamba kura iliyokuwa ikingojwa kuhusu makubaliano yake ya Brexit na Umoja wa Ulaya imekuwa haina tena maana.

Lakini ameongeza: "Jambo bora kwa Uingereza na kwa Ulaya yote ni kujitoa kwa kutumia mpango huu mpya Oktoba 31."

"Sitafanya mazungumzo na Umoja wa Ulaya ya kuchelesha, na wala sheria hainilazimishe kufanya hivyo," alisema.

Sheria tofauti iliyopitishwa mwezi uliopita inamlazimu Johnson kuuandikia barua Umoja wa Ulaya ya kuomba aongezewe muda iwapo mpango haujapitishwa Oktoba 19.

Soma zaidi: Juncker: Hali kuwa tata zaidi wabunge wa Uingereza wakikataa mkataba wa Brexit

Johnson mapema alidai kwamba kuchelewesha zaidi - miaka mitatu baada ya kura ya maoni ya mwaka 2016 kujiondoa katika umoja huo - itakuwa hatua "isiyo na maana, na yenye gharama kubwa".

Umoja wa Ulaya umeihimiza Uingereza kuweka wazi mipango yake mapema iwezekanavya, huku kiongozi wa chama cha upinzani Labour, Jeremy Corbyn, ambaye chama chake kinapinga mpango huo wa Johnson, amesema: "Waziri Mkuu lazima sasa azingatie sheria."

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com