Waasi wa Syria maji ya shingo,Obama aahidi kuwasaidia silaha. | Matukio ya Kisiasa | DW | 14.06.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Waasi wa Syria maji ya shingo,Obama aahidi kuwasaidia silaha.

Licha ya kutangazwa kwa azma hiyo ya Marekani, Ikulu ya White House imeweka wazi kwamba, Rais Assad amevuka kile Obama alichowahi kukiita "mstari mwekundu", serikali hiyo inakusudia kuliendelea suala hilo kwa tahadhari.

Rais wa Marekani Barack Obama

Rais wa Marekani Barack Obama

Uamuzi wa Rais Obama wa kuwapelekea silaha waasi unakuja wakati vikosi vya Assad, vikisaidiwa na Hizbullah, vikisonga mbele kuelekea ngome kuu ya waasi, mji wa kaskazini wa Aleppo.

Tayari kuna kila dalili za kushindwa kwa waasi nchini Syria, kufuatia msaada huo wa Hizbullah, kwani hivi karibuni wamepoteza mji muhimu wa Qusayr. Naibu mshauri wa usalama wa Marekani, Ben Rhodes, amesema kwamba Rais Obama ameamua tu kutoa msaada wa kijeshi, bila ya kuweka wazi ukubwa na upana wa msaada huo.

Hata hivyo, uamuzi huu unaashiria kuhama kwa msimamo wa Marekani kutoka ule wa kuangalia mambo na kuja wa kuingilia mambo, ambao imeuchukua kwa muda mrefu, ikihofia kujirejea kwa hali ya Libya na pia maslahi yake muhimu kwa taifa jirani la Syria, Israel.

Maafisa wa serikali ya Obama wamesema ikiwa waasi watapewa silaha hizo, basi zitakuwa ni zile ndogo ndogo na sio makombora ya kutungulia ndege, kama ambavyo wameomba, na ambayo yatakuwa na matokeo ya haraka kwenye vita vyao dhidi ya Assad.

Gazeti la New York Times limeripoti kwamba utumwaji wa silaha hizo utaratibiwa na Shirika la Ujasusi la Marekani, CIA, na huenda ukajumuisha silaha za kukabiliana na vifaru vya kijeshi.

Utawala wa Assad unatumi silaha za sumu

rais wa Syria Bashar al-Assad

rais wa Syria Bashar al-Assad

Wakati Marekani ikisema kuwa ina uhakika kuwa Assad ametumia silaha za sumu, mwanasheria wa ngazi za juu kwenye ikulu ya Urusi, Kremlin, amesema hivi leo kuwa taarifa hizo zilitungwa ili Marekani izitumie kuhalalisha uingiliaji wake kati kwenye mzozo huo.

Mkuu huyo wa kamati ya sera za mambo ya nje, Alexei Pushkov, amesema na hapa namnukuu: "Taarifa za Assad kutumia silaha za kemikali zimetungwa pale pale ulipotungwa uongo kuhusu Saddam Hussein kumiliki silaha za maangamizi. Obama anafuata njia ile ile ya George Bush," mwisho wa kumnukuu.

Bado haijafahamika Urusi itachukua hatua gani kama Marekani itatekeleza kweli azma yake ya kuwapa silaha waasi wa Syria.

Kuingia kwa maelfu ya wanamgambo wa kundi la Hizbullah la Lebanon, linaoungwa mkono na Iran, kwenye vita hivyo, kunatajwa kuwa miongoni mwa sababu za kubadilika kwa msimamo wa Marekani. Hadi sasa, Umoja wa Mataifa unakisia kuwa watu 93,000 wameshauawa nchini Syria tangu vita vianze zaidi ya miaka miwili iliyopita.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters

Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com