1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

M23 yakaribia Uvira, wanajeshi wa Kongo wakimbilia Burundi

9 Desemba 2025

Waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wanaendelea kusonga mbele katika uwanja wa mapambano huko mashariki mwa Kongo na kukaribia kuchukua udhibiti wa mji wa Uvira unaopakana na nchi jirani ya Burundi.

https://p.dw.com/p/54zKI
DRCongo I Wananchi wakikimbia mapigano mashariki mwa Kongo
Wananchi wa DRC wakikimbia mapigano mashariki mwa Kongo kati ya M23 na jeshi la FARDCPicha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Taarifa zinaeleza kuwa mamia ya wanajeshi wa Burundi na Kongo wamelazimika kukimbilia nchini Burundi. Wizara ya mambo ya nje ya Burundi imelaani kile ilichokiita uchokozi wa Rwanda, kwa kudai kuwa Kigali ilifanya mashambulizi ya makombora Jumatatu usiku karibu na mkoa wa Cibitoke na kuwajeruhi watu wawili, akiwemo mtoto mwenye umri wa miaka 12.

Vurugu zimeongezeka eneo hilo ikiwa ni siku chache tu baada ya kusainiwa kwa makubaliano ya amani kati ya  Rwanda na DRC yaliyosimamiwa na Marekani, huku rais wa Kongo Felix Tshisekedi akimtuhumu mwenzake wa Rwanda Paul Kagame kwa kukiuka makubaliano hayo.