Waasi Sudan Kusini wanapambana kuutwa tena mji wa Bor | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.12.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Waasi Sudan Kusini wanapambana kuutwa tena mji wa Bor

Waasi Sudan Kusini wanaomtii aliyekuwa makamu wa raisi wa nchi hiyo, Riek Machar, wanapambana kuutwaa tena mji muhimu ambao walilazimishwa kuukimbia wiki iliyopita baada ya mapambano makali na vikosi vya serikali.

Wanajeshi wa UNMISS

Wanajeshi wa UNMISS

Waasi Sudan Kusini wanaomtii aliyekuwa makamu wa raisi wa nchi hiyo, Riek Machar, wanapambana katika juhudi za kuutwaa tena mji muhimu ambao walilazimishwa kuukimbia wiki iliyopita baada ya mapambano makali na vikosi vya serikali.

Msemaji wa jeshi la Sudan Kusini, Kanali Philip Aguer, amesema kuwa majeshi tiifu kwa Machar leo (30.12.2013) yanaelekea katika mji wa Bor, lakini wana uhakika kwamba watawafukuza na kuulinda mji huo.

Riek Machar na Rais Salva Kiir

Riek Machar na Rais Salva Kiir

Alisema mapigano makali yalizuka jana Jumapili (29.12.2013) katika eneo la Gadiang lililoko kaskazini mwa mji wa Bor na wakaazi wa eneo hilo wanahofia kuzuka kwa mashambulizi wakati wowote ule.

Hata hivyo, taarifa hizo zinakanganya kutokana na taarifa iliyotolewa jana jioni na msemaji wa serikali ya Sudan Kusini, Michael Makuei kwamba waasi walikuwa wameanza kurejea makwao baada ya kusitisha hatua ya kuingia kwenye mji huo wa Bor.

Madai ya kuwepo vijana wanaotaka kufanya mashambulizi

Umoja wa Mataifa jana ulisema kuna wasiwasi mkubwa kuhusu madai ya kuwepo zaidi ya vijana 25,000 wenye silaha wanaojitayarisha kuushambulia mji wa Bor, ambao ni mji mkuu wa jimbo la Jonglei.

Makuei alisema kulingana na vyanzo vyake vya habari, viongozi wa makabila ya Lou na Dau Nuer waliwashawishi vijana hao kuweka chini silaha na kurejea nyumbani. Hata hivyo, hakuna uthibitisho kwamba vijana hao wanaomuunga mkono Machar wamesitisha hatua hiyo.

Taarifa ya Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa kikosi cha kulinda amani cha umoja huo nchini Sudan-UNMISS kinafatilia harakati za vijana hao wenye silaha za kivita wanaojiita ''Jeshi Jeupe'', lakini hakiwezi kuthibitisha ukubwa wake au eneo waliko. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, UNMISS, imefanya uchunguzi kwa kutumia ndege na kubaini kuwa kundi hilo liko umbali wa kilomita 50 kaskazini-mashariki mwa Bor.

Mkuu wa UNMISS, Hilde Johnson ambaye baadae leo atalipa taarifa fupi Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Sudan Kusini, amekuwa akijitahidi kuwashawishi viongozi wa kisiasa na kikabila kusitisha hatua za vijana hao kusonga mbele na kwenda Bor.

Mkuu wa UNMISS, Hilde Johnson

Mkuu wa UNMISS, Hilde Johnson

Juhudi za kimataifa kumaliza mapigano

Wakati huo huo, juhudi za kimataifa zinaendelea ili kusitisha mapigano hayo yaliyoanza baada ya Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini kudai kuwa Machar alifanya jaribio la kuipindua serikali yake. Hata hivyo, Kiir amesema yuko tayari kwa mazungumzo na Machar.

Lakini jana Jumapili, Makuei alisema ana wasiwasi iwapo watafanya mazungumzo na Machar kwa sababu alikaidi wito ulitolewa na viongozi wa Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Mashariki na Pembe ya Afrika-IGAD na Umoja wa Afrika wa kusitisha mapigano.

Zaidi ya watu 1,000 wameuawa tangu kuzuka kwa mapigano kati ya vikosi vya serikali na vile vya Machar na kwamba kiasi watu 180,000 hawana makaazi na wengine 75,000 wamepatiwa hifadhi katika ofisi za Umoja wa Mataifa.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,APE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com