1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita dhidi ya Boko Haram vinavyoathiri upatikanaji chakula

16 Oktoba 2017

Mapigano dhidi ya kundi la kigaidi la Boko Haram kaskazini mwa Nigeria yamedumu kwa miaka saba sasa, na licha ya kuwa kwake vita vya kijeshi, ukweli ni kuwa vinaathiri sana hali ya upatikanaji chakula.

https://p.dw.com/p/2lZYY
Der Hunger in Rann ist überall sichtbar
Picha: DW/A.Kriesch

Goni Abba ni mkulima na anaelekea katika shamba lake. Ni msimu wa mvua kaskazini mwa Nigeria na kwa sasa ni sharti atayarishe kila kitu na anyunyize dawa ya kuzuia wadudu. Katika eneo la Rann, alikuwa hawezi kwenda nje kutokana na hali tete ya usalama.

"Ni lazima tuwAachie Boko Haram mashamba yote yaliyo nje. Hapa kuna usalama kidogo lakini hakuna ardhi ya kututosheleza," anasema Abba.

Hii ni mara ya kwanza kabisa ambapo Abba anapata fursa ya kufanya ukulima tena. Mwaka uliopita baba huyo aliacha kabisa kuhesabu siku ambazo hajatia chochote mdomoni na kwa mwaka ujao hana matumaini kabisa.

"Mavuno haya hayatonifikisha mbali. Nina wake wawili na watoto tisa ambao lazima niwalishe. Kwa mwaka, ninahitaji karibu magunia 40 ya mawele ili niweze kuuvuka msimu na kufikia mwengine. Lakini angalia hili shamba. Nina bahati babu yangu aliniachia lakini bado niko mbali sana kulifikia lengo langu."

Ulinzi wa jeshi

Jeshi la Nigeria linalilinda eneo hilo la Rann na wakaazi wanakubaliwa kutembea umbali wa kilomita tano tu. Katika eneo lililo karibu na shamba la Abba, maafisa wa usalama ambao hawajapewa mafunzo ya kutosha ndio wanaotoa ulinzi.

"Tunapiga doria katika eneo hili usiku na mchana. Tunapokutana na wanamgambo wa Boko Haram, tunapambana nao. Ama tuwaue wao au watuuwe sisi. Hatuogopi chochote. Sisi wenyewe tunapoona mwangaza wakati wa usiku popote, tunakwenda mara moja na kuangalia kilichoko," anasema Mohammed Abba Yai, mmoja wa wanajeshi hao wanaopambana na Boko Haram.

Hungersnot in Nigeria
Kitoto kikipimwa uzito na kusaidiwa matibabu ya utapiamlo nchini Nigeria.Picha: picture alliance/dpa/Unicef/NOTIMEX

Mavuno yanapofeli athari zake zinaonekana wazi kila mahali. Watu wengi wanakabiliwa na njaa na ukosefu wa chakula.

Na kwa sasa kwa vile ni msimu wa mvua, mashirika ya kutoa misaada yameweka mipaka ya maeneo yanayofika kwasababu njia hazipitiki katika eneo hilo la Rann.

Mtaalamu wa masuala ya usalama, Peter Lundberg, anasema kilichopo Nigeria ni mzozo wa kiusalama ambao umepindukia na kuwa mzozo wa chakula. "Ni hali tete mno na tuko katika kilele cha mwaka wa matatizo. Tunasubiri na tuna matumaini kwamba mbegu, vifaa vya ukulima na mbolea ambavyo vinatumiwa kuwaunga mkono wakulima, vitapelekea kutolewa kwa mazao mazuri na yafanye hali kuwa nzuri."

Matumaini madogo

Wengi katika eneo hili hawawezi kuangalia maisha ya mbeleni kwa matumaini. Mtaalamu wa masuala ya kilimo nchini Nigeria, Abba Gambo, anaishutumu serikali kwa kutowaunga mkono wakulima na anatoa wito wa kutolewa vyakula vya kutosha vya misaada.

"Iwapo unawapa watu mbegu lakini hakuna chakula, basi kimahesabu inamaanisha kwamba watakula hizo mbegu. Iwapo mtu mwenye njaa ana kilo kumi za mawele katika shamba lake na nyumbani kwake ana wake wawili na watoto saba bila shaka watakuwa na njaa na itamuuma sana mwanamume huyo kwa kutoweza kuwapa wanawe chakula," anasema Gambo.

Bila amani, mkulima Goni Abba hafahamu iwapo njaa itakwisha. Majirani zake wengi hawawezi kutumia mashamba yao kwa sasa ambapo ni msimu wa mvua na kwa mwaka mwengine watakuwa wanapokea misaada ya chakula. 

Mwandishi: Adrian Kirsch
Tafsiri: Jacob Safari
Mhariri: Mohammed Khelef