Visa vya mateso vyaongezeka Burundi | Matukio ya Afrika | DW | 19.04.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Visa vya mateso vyaongezeka Burundi

Kamishna wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya haki za binaadamu, ameonya kwamba kuna ongezeko kubwa la watu kuteswa Burundi, akisema kuna visa vipya 345 vilivyoripotiwa tangu mwanzoni mwa mwaka huu.

UN Kommissar für Menschenrechte Zeid Ra'ad Al Hussein

Kamishna wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya haki za binaadamu, Zeid Ra'ad Al Hussein

Zeid Ra'ad Al Hussein amesema kuongezeka kwa visa hivyo, ni ishara ya wazi kuwa vikosi vya serikali vinaendelea kutumia mbinu ya mateso dhidi ya raia, huku akielezea wasiwasi juu ya kuwepo vituo vya siri ambavyo serikali inatumia kuwazuilia watu.

Zeid ameelezea wasiwasi wake juu ya kuongezeka kwa mashambulizi yanayofanywa na makundi ya watu wenye silaha wasiojulikana, wanaofungamanishwa na makundi ya waasi na kulaani hatua ya kuwalenga wanachama wa chama tawala katika mashambulizi hayo.

Kamishana huyo wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia haki za binaadamu, amesema mateso makubwa nchini humo yanafanyika katika vituo vinayoendeshwa na kitengo cha Ujasusi, polisi pamoja na jeshi. Ameongeza kuwa wale wanaotekeleza mateso hayo wanaendelea kulindwa.

Burundi Militärputsch

Baadhi ya vikosi vya usalama Bujumbura, Burundi

Hata hivyo ziara fupi iliyofanywa na maafisa wa Umoja wa Mataifa wanaoshughulikia haki za binaadamu katika vituo vya kuzuilia watu vinayoendeshwa na kitengo hicho cha ujasusi mjini Bujumbura, iligundua watu 30 kati ya 67 waliyokuwepo huko, walionyesha dalili za mateso.

Wengi walikuwa na majeraha mwilini, wengine hawakuweza kutembea bila kusaidiwa baada ya kupigwa kwa kutumia mikanda, nyaya ama vifaa vilivyo na ncha kali.

Ban Ki Moon asema hali ya Burundi ni ya hatari

Aidha Al Huusein ameitolea mwito serikali ya Burundi kukomesha haraka mateso hayo yasiokubalika. Matamshi ya Al Hussein yamekuja siku moja baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon kuelezea hali nchini Burundi kuwa ya hatari na kupendekeza hatua kadhaa kwa ujumbe mpya wa Usalama wa Umoja wa Mataifa utakaopelekwa huko.

Ban Ki Moon amependekeza kupeleka kati ya polisi 20 hadi 3000 nchini Burundi, ambapo hali ya kisiasa imekuwa tete kwa mwaka mzima sasa, lakini akadokeza kuwa serikali imeonyesha dalili ya kuchukua wataalamu 20 pekee wasiokuwa na silaha.

UN - Ban Ki-moon im Irak

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon

Kwa hilo kutendeka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linabidi lipitishe azimio jengine la kuridhia polisi kupelekwa nchini Burundi. Ban amesema ushirikiano wa hali ya juu kutoka kwa serikali ya Burundi utahitajika kuhakikisha ufanikishaji wa kikosi chochocte cha usalama.

Burundi imekumbwa na machafuko tangu mwezi Aprili mwaka wa 2015 wakati rais Pierre Nkurunziza alipotangaza nia yake ya uwania muhula wa tatu madarakani hatua ambayo upinzani uliipinga na kusema kuwa ni kinyume cha katiba. Tangu machafuko kuanza nchini humo watu zaidi ya 400 wameuwawa huku wengine zaidi ya 250,000 wakiachwa bila makao na wengine kukimbilia nchi jirani.

Mwandishi: Amina Abubakar/AP/AFP/REUTERS

Mhariri: Yusuf Saumu