1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Mali wajiuzulu kufuatia mapinduzi ya kijeshi

Grace Kabogo
26 Mei 2021

Viongozi wa mpito wa Mali wamejiuzulu kama sehemu ya juhudi za upatanishi, baada ya kuwekwa kizuizini katika mapinduzi ya kijeshi ya pili kutokea ndani ya kipindi cha miezi tisa.

https://p.dw.com/p/3u02U
Mali | Übergangspräsident | Bah N'Daw trifft Moctar Ouane
Picha: Boubou Doucouré/DW

Baba Cisse, mshauri wa kiongozi wa kijeshi Kanali Assimi Goita amesema Rais Bah Ndaw na Waziri Mkuu Moctar Ouane wamejiuzulu kabla ya upatanishi. Ndaw na Ouane walikuwa na jukumu la kuiongoza serikali ya mpito iliyowekwa mwezi Agosti mwaka uliopita na kuhakikisha kurejea kwa utawala wa kiraia baada ya mapinduzi.

Mazungumzo yanaendelea

Cisse amesema mazungumzo yanaendelea kwa ajili ya viongozi hao kuachiliwa huru na kuundwa kwa serikali mpya ya Mali. Mjumbe wa timu ya upatanishi chini ya Jumuiya ya Uchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, amelithibitisha shirika la habari la Ufaransa, AFP kuwa Rais Ndaw amejiuzulu.

Mapema Jumatano, ujumbe huo wa ECOWAS ulienda katika kambi ya kijeshi ya Kati iliyoko umbali wa kilomita 15 na mji mkuu Bamako, kuwatembelea viongozi hao wawili walioko kizuizini.

Kanali Goita ambaye anashikilia nafasi ya Makamu wa Rais anawashutumu Ndaw na Ouane kwa kukiuka hati ya makubaliano kuhusu serikali ya mpito na kushindwa kuwasiliana naye kuhusu kufanya mabadiliko ya baraza la mawaziri, ambapo maafisa wawili wa kijeshi walipoteza nafasi zao.

Mali I Nationalfeiertag in Bamako
Kiongozi wa kijeshi wa Mali, Kanali Assimi GoitaPicha: Michele Cattani/AFP/Getty Images

Kiongozi huyo wa kijeshi pia anawashutumu Ndaw na Ouane kwa kushindwa kuituliza hali ya mambo nchini Mali, ukiwemo mgomo wa wiki iliyopita ulioandaliwa na shirikisho la vyama vya wafanyakazi. Siku ya Jumanne, shirikisho hilo lilisema litasitisha mgomo wake kwa kuzingatia hali ya mzozo wa kisiasa.

Siku ya Jumatatu Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, ECOWAS, Umoja wa Ulaya na Marekani zilitoa taarifa ya pamoja kulaani kitendo hicho na kutoa wito kwa viongozi hao kuachiwa mara moja bila masharti yoyote yale.

Umoja wa Mataifa kukutana

Nalo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakutana Jumatano kwa mazungumzo ya dharura na faragha kuhusu Mali. Mkutano huo umependekezwa na Ufaransa, Niger, Tunisia, Kenya pamoja na Saint Vincent na Grenadines.

Mwaka uliopita, maafisa vijana wa jeshi walimuondoa madarakani Rais Ibrahim Boubacar Keita, baada ya wiki kadhaa za maandamano kuhusu ufisadi serikali na kushindwa kupambana na mashambulizi ya wapiganaji wa jihadi.

Nchi jirani na Mali na jumuia ya kimataifa zina wasiwasi kwamba mzozo wa kisiasa unaweza kusababisha kukosekana zaidi kwa utulivu kwenye nchi hiyo ambayo makundi yenye itikadi kali za Kiislamu yenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda na kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS zimeitumia kama eneo la kupanga mashambulizi katika ukanda huo.

(AFP, Reuters)