Ulimwengu waungana kulaani shambulio la kigaidi Bondi Beach
14 Desemba 2025
Shambulio la risasi lililotokea Jumapili katika ufukwe maarufu wa Bondi Beach mjini Sydney limezua mshtuko na hasira duniani kote. Watu wasiopungua 12 waliuawa katika tukio hilo lililotokea wakati wa maadhimisho ya sikukuu ya Kiyahudi ya Hanukkah.
Waziri Mkuu wa Australia, Anthony Albanese, alilitaja shambulio hilo kuwa la kushtua na la kuhuzunisha. Alisema ni tukio lisiloelezeka na lililotangazwa rasmi na polisi kuwa shambulio la kigaidi.
Rais wa Israel, Isaac Herzog, alilaani tukio hilo akisema ni shambulio katili dhidi ya Wayahudi. Aliwataja wahusika kama magaidi waovu waliolenga raia wasio na hatia.
Mfalme Charles wa Tatu, mkuu wa Jumuiya ya Madola, alisema ameshtushwa na kile alichokiita shambulio baya zaidi la kigaidi lenye chuki dhidi ya Wayahudi. Alitoa pole kwa waathiriwa na familia zao.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, alisema chuki dhidi ya Wayahudi haina nafasi duniani. Alisema mawazo na maombi ya Wamarekani yako pamoja na waathiriwa na watu wa Australia.
Mkuu wa Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, alisema ameshtushwa na kitendo hicho cha vurugu. Alisisitiza kuwa Ulaya inasimama pamoja na Australia na jamii za Kiyahudi kote duniani.
Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, alisema alipokea kwa masikitiko makubwa taarifa za shambulio hilo. Alitoa rambirambi kwa familia za waathiriwa na jamii yote iliyoathiriwa.
Ugaidi na mauaji ya binadamu havikubaliki popote
Iran, ambayo ni adui mkubwa wa Israel, pia ililaani shambulio hilo. Wizara ya mambo ya nje ya Iran ilisema ugaidi na mauaji ya binadamu hayakubaliki popote pale.
Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, alisema Ufaransa itaendelea kupambana bila kuchoka dhidi ya chuki ya Kiyahudi. Alieleza mshikamano wake na waathiriwa wa shambulio hilo.
Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni, alisema alipokea kwa huzuni kubwa taarifa za vifo vya Sydney. Alisisitiza kuwa Italia inalaani aina zote za vurugu na chuki dhidi ya Wayahudi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Johann Wadephul, alisema ameshtushwa sana na shambulio hilo. Alilitaja kama kitendo cha chuki kilicholenga Wayahudi duniani kote siku ya kwanza ya Hanukkah.
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskiy, alisema nchi yake inasimama bega kwa bega na Australia. Alisisitiza kuwa ugaidi na chuki lazima zishindwe kila mahali.
Nchini Australia, Baraza la Kitaifa la Maimamu pia lililaani shambulio hilo. Lilitoa wito kwa Waaustralia wote kusimama pamoja kwa umoja na mshikamano.
Baraza hilo la Kiislamu liliwataka raia kuonyesha huruma kwa waathiriwa na familia zao. Lilisema vurugu hizo zimeacha majeraha makubwa ya kisaikolojia.
Kwa upande mwingine, mkuu wa Jumuiya ya Wayahudi Australia, Robert Gregory, alisema shambulio hilo lilikuwa janga lililotarajiwa.
Alidai serikali ilikuwa imeonywa mara kadhaa lakini haikuchukua hatua za kutosha kulinda jamii ya Wayahudi.