1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UN-Menschenrechtsrat in Genf Schweiz
Picha: picture-alliance/Photoshot/Xu Jinquan

Venezuela yajishindia kiti katika Baraza la Haki za Binadamu

John Juma
18 Oktoba 2019

Venezuela imeshinda kiti ya kuwa katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa. Hata hivyo ushindi huo umeshutumiwa na mataifa pamoja na wanadiplomasia kadhaa kufuatia rekodi ya nchi hiyo kuhusu haki za binadamu.

https://p.dw.com/p/3RVS0

  Venezuela imeshinda kiti katika baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa. Ushindi wa Venezuela katika uchaguzi huo uliokumbwa na utata, umepatikana licha ya zaidi ya mashirika 50 pamoja na mataifa yanayoipinga serikali na rekodi ya Rais Nicolas Maduro kuhusu haki za binadamu kuipinga Venezuela.

Kulikuwa na ushangiliaji mdogo sana katika baraza kuu la Umoja wa Mataifa wakati rais wake alipotangaza ushindi wa Venezuela miongoni mwa nchi mbili za Amerika ya Kusini kuwa katika baraza la haki za binadamu, ambapo Brazil ilishinda kwa kura 153 na ikafuatiwa na Venezuela iliyopata kura 105, Costarica ikishika nafasi ya tatu kwa kura 96.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Venezuela, Jorge Arreaza amesema kura hiyo ni "ushindi uliopatikana" baada ya kampeni kali kutoka kwa Marekani na washirika wake dhidi ya Venezuela.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Kelly Craft ameitaja hatua ya kuiruhusu serikali ya Venezuela kuwa katika baraza la haki za binadamu kuwa dhihaka kubwa kwa Umoja wa Mataifa na janga kwa raia wa Venezuela.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Kelly Craft akizungumza katika mkutano wa Baraza Kuu la usalama la Umoja wa Mataifa 19.09.2019
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Kelly Craft akizungumza katika mkutano wa Baraza Kuu la usalama la Umoja wa Mataifa 19.09.2019Picha: UN Security Council Chamber/Cia Pak

Guaido ataka Umoja wa Mataifa ujichunguze

Naye Juan Guaido, ambaye ni kiongozi wa upinzani unaoongoza bungeni Venezuela ameukashifu ushindi huo. Amesema Umoja wa Mataifa umechafuliwa na kura hiyo na umepoteza uaminifu wake.

''Wale wanaopaswa kujichunguza ni Umoja wa Mataifa. Inawezekanaje kwa nchi inayochunguzwa kwa kukiuka haki za binadamu, na ripoti moja yenye nguvu kihistoria dhidi yake, kuwa na nafasi ambayo sasa inashikiliwa na udikteta. Lazima kuangalia hili kwa uwazi.'' Amesema Guaido.

Kwenye taarifa yake baada ya kura hiyo, balozi Craft amesema kwamba taifa lenye wavunjaji wakubwa wa haki za binadamu kupewa kiti katika baraza linalopaswa kutetea haki za binadamu, ni jambo linalosikitisha zaidi.

Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Brazil imesema kuchaguliwa kwao tena ni ishara ya ushindi muhimu. Lakini imekosoa kuchaguliwa kwa Venezuela katika baraza hilo.

Rais wa Venezuela Nicolas Maduro
Rais wa Venezuela Nicolas MaduroPicha: Getty Images/AFP/Y. Cortez

Kwenye taarifa, wizara hiyo imeongeza kuwa kuchaguliwa kwa Venezuela ni dhihirisho kuwa bado kuna kazi kubwa inayohitajika ya uhamasishaji kimataifa kuhusu hali mbaya ya haki za binadamu nchini Venezuela.

Balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa, Danny Danon amesema kupitia taarifa baada ya matokeo ya kura hiyo kutangazwa kuwa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa linaendelea kuacha kutetea haki za binadamu na sasa limejikita katika kuwalinda madikteta na wahalifu wa kivita.

Utawala wa Trump unamuunga mkono Guaido

Hata hivyo maafisa wa Venezuela mara kwa mara hukana ukosoaji wowote dhidi ya rekodi ya nchi hiyo kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu.

Utawala wa Donald Trump umemtambua kiongozi wa upinzani nchini Venezuela Juan Guaido kama rais wa mpito.

Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa lina jumla ya nchi wanachama 47 zinazohudumu kwa muda wa miaka mitatu kuanzia Januari mosi. Viti hushindaniwa kulingana na kanda mbalimbali za ulimwengu ili kuwe na sura ya uwakilishi ulimwenguni kote.

Marekani ilijiondoa kwa kiasi fulani kutoka kwenye baraza hilo lililoasisiwa mwaka 2006 na ambalo makao yake makuu ni Geneva, kwa sababu ililitizama baraza hilo kama jukwaa la watu wanafiki kuhusu haki za binadamu, lakini pia kwa sababu Marekani ilisema baraza hilo linaipinga Israel.

Vyanzo: AP