1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Venezuela washindwa kuafikiana

Lilian Mtono
30 Mei 2019

Mazungumzo ya kumaliza mzozo wa kisiasa nchini Venezuela yameingia katika mkwamo, baada ya wawakilishi wa serikali ya Venezuela na upinzani kushindwa kufikia makubaliano nchini Norway.

https://p.dw.com/p/3JUuC
Venezuela Krise l selbsternannter Interimspräsident Juan Guaidó spricht bei einer Kundgebung in Carora
Picha: picture-alliance/dpa/L. Fernandez

Hata hivyo kiongozi wa upinzani Juan Guaido amesema mazungumzo hayo yataendelea licha ya mjadala wa jana Jumatano kumalizika bila maafikiano.

Taarifa iliyotolewa na wawakilishi wa Juan Guaido  aliyejitangaza rais wa mpito imethibitisha majadiliano hayo kumalizika bila ya kuafikiana. Kulingana na taarifa hiyo upinzani umeendelea kusalia kwenye masharti yake ya kumtaka rais Nicolas Maduro kujiuzulu, kuanzishwa kwa serikali ya mpito na kufanyika uchaguzi huru.

Kwenye mahojiano na kituo cha televisheni cha Fox News cha nchini Marekani hapo jana, Guaido alisema, upo uwezekano wa kuendelea kwa maandamano baada ya mazungumzo hayo kushindwa kutoa makubaliano, alisema, "Ndio, tunataka kupata suluhu ya mzozo na tutakuwepo katika majadiliano yoyote.. hakukua na makubaliano ya haraka, kwa hiyo fursa ambayo tunayo kwa wakati huu ni kusalia mitaani."

Venezuela Krise l Anti-Regierungsprotest - Guaido Unterstützer
Guaido ameahidi kusalia mitaani, bada ya mazungumzo hayo kukosa muafakaPicha: Getty Images/AFP/F. Parra

Serikali ya Maduro, ambayo hata hivyo haikuthibitisha kuhusu kushindwa kwa mazungumzo hayo ya Oslo baadae ilielezea nia yake ya kuendelea na majadiliano na upinzani. Rais Maduro amesema kwenye taarifa yao kuwa wanapendelea kufuata mkondo wa majadiliano, umoja wa kitaifa, kuheshimu katiba na suluhu ya tatizo lililopo. 

Maduro, kiongozi anayekabiliwa na changamoto lukuki, aliongeza kuwa asilimia 80 ya Wavenezuela wanaunga mkono majadiliano, huku wachache wakiwa wanaamini katika mapinduzi na uvamizi wa kijeshi matamshi yaliyohusishwa na uwezekano wa Marekani kujiingiza kijeshi nchini humo.

Wizara ya mambo ya kigeni ya Norway ilisema kwamba pande hizo mbili zimejadili masuala kuhusu siasa, uchumi na uchaguzi, lakini pia zimeonyesha utayari wao wa kusonga mbele katika kusaka suluhu baina yao na ya kikatiba.

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imeendelea kusisitiza kwamba kitu pekee wanachotakiwa kukubaliana na Maduro ni kuhusu mazingira ya kuondoka kwake madarakani.

Wajumbe wa mazungumzo hayo wamekutana ana kwa ana kwa mara ya kwanza jana mjini Oslo katika mchakato ulioanza wiki mbili zilizopita chini ya usimamizi wa Norway kijadili kuhusu mzozo wa kisiasa na kiuchumi unaolikabili taifa hilo la Amerika ya Kusini.