1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya amani ya Venezuela huko Oslo yatoa tumaini

Yusra Buwayhid
16 Mei 2019

Wawakilishi wa upande wa serikali ya Venezuela na wa upinzani wamekutana kwa mazungumzo ya amani katika eneo la siri la mjini Oslo, Norway. Mazungumzo hayo yana nia ya kumaliza mgogoro wa kisiasa wa miezi mitano.

https://p.dw.com/p/3IcIu
Venezuela politische Krise Oppositionsanhänger
Picha: Getty Images/E. M. Uzcategui

Venezuela imetumbukia katika mzozo wa kisiasa tangu spika wa bunge la taifa hilo, Juan Guaido, kujitangaza kuwa rais wa mpito mwezi Januari, hatua inayoashiria upinzani mkubwa kwa utawala wa Rais wanchi hiyo Nicolas Maduro.

Shirila la redio na televisheni Norway la NRK, limenukuu duru ambazo hazikutajwa kwa majina, na kusema kwamba mazungumzo hayo ya amani yalifanyika katika sehemu ya siri mjini Oslo kwa siku kadhaa na wajumbe wa pande zote mbili wanatarajiwa kurudi mji mkuu wa Venezuela, Caracas, Alhamis.

Ni mara ya pili kwa mazungumzo ya aina hiyo kufanyika mjini Oslo, kati ya wawakilishi wa serikali ya Maduro na wa Guaido, limesema shirika la NRK, nakuongeza kwamba mazungumzo pia yalifanyika nchini Cuba.

Norway yakataa kuthibitisha kuhusika na mazungumzo 

"Hatuwezi kuthibitisha wala kukana kuhusika katika mchakato wa amani au mipango ya majadiliano," msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Norway Anne Haavardatter, ameliambia shirika la habari la AFP.

Mashirika mengine kadhaa ya Amerika Kusini pia yameripoti kuhusu mazungumzo hayo yaliyofanyika nchini Norway.

Waziri wa Mawasiliano Venezuela Jorge Rodriguez na gavana wa jimbo la Miranda Hector Rodriguez, waliuwakilisha upande wa serikali ya Maduro kwa mujibu wa vyombo vya habari.

Upande wa upinzani uliwakilishwa na naibu wa zamani Gerardo Blyde, waziri wa zamani Fernando Martinez Mottola na Makamu wa Rais wa Bunge Stalin Gonzalez.

Venezuela: Juan Guaido in Caracas
Kiongozi wa upinzani Venezuela, Juan GuaidoPicha: Getty Images/E. Uzcategui

Kuna matamshi kadhaa yanayochochea fununu hizo za mkutano wa Norway. Mjini Caracas kwa mfano, Maduro amesema kwamba Jorge Rodriguez ametumwa nje ya nchi kwa shughuli muhimu.

Guaido kwa upande wake ameandika katika ukurasa wake wa kijamii wa Twitter, "Kundi la Contact -la nchi zenye nguvu duniani na zenye maslahi makubwa katika nchi za Balkani- Canada, Uingereza, Norway, kundi la Lima pamoja na makundi mengine yanasaidia kutafuta suluhisho la mgogoro wa Venezuela."

Mataifa 50 yamuuunga mkono Guaido

Guaido, spika wa bunge la Venezuela linalohodhiwa na upinzani, amekuwa akivutana na Maduro, ambaye amelitumbukiza taifa hilo kwenye mgogoro mkubwa wa kisiasa na kiuchumi tangu alipompokea madaraka kiongozi wa siasa za mrengo wa kushoto Hugo Chaver mwaka 2013.

Maduro alichaguliwa tena kwa muhula wa pili wa uongozi Mei 2018, katika uchaguzi uliosusiwa na upinzani na kukataliwa na mataifa mengi katika jumuiya ya kimataifa.

Guaido alijitangaza rais wa mpito Januari 23, na kusema uchaguzi wa Maduro haukuwa halali. Tangu wakati huo, kiongozi huyo wa upinzani ametambuliwa na zaidi ya mataifa 50, ikiwamo Marekani inayomuunga mkono kwa karibu zaidi.

Norway hata hivyo imetowa wito wa kuitishwa uchaguzi mpya na huru nchini Venezuela, tamko linaloashiria kuwa ingetaka kuchukua nafasi ya mpatanishi kati ya pande hizo mbili zinazovutana.

Mbali na mgogoro wa kisiasa, uliogubikwa na mapigano yaliyochukua maisha ya watu wengi, Venezuela imekabiliwa na mgogoro mkubwa zaidi wa kiuchumi kuwahi kushuhudiwa miaka ya karibuni. Robo ya wakaazi wake wanahitaji msaada wa dharura wa kibinadamu, kulingana na Umoja wa Mataifa.