Utata kuhusu uchaguzi mkuu nchini Kenya
19 Machi 2012Tume Huru ya Uchaguzi nchini Kenya IEBC imetangaza kuwa uchaguzi utafanyika tarehe 4 Machi 2013, baada ya Rais Mwai Kibaki na Waziri Mkuu Raila Odinga kushindwa kuafikiana juu ya tarehe ya uchaguzi huo. Kwa mujibu wa Barack Muluka, mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Kenya, tarehe iliyotangazwa na tume ya uchaguzi inaendana na maelekezo ya katiba na sheria za nchi, lakini licha ya hivyo, kunaonekana kuwepo kwa ukiukwaji wa sheria,anavyosema mchambuzi huyo ni kwamba''.
“kwa kiasi kikubwa (IEBC) wameweza kukiuka sheria na kuvunja mbarika kabla wakati haujawadia. Ni lazima bunge liwe limevunjwa ndipo wanapoweza kutangaza tarehe ya uchaguzi, na ni kwa mwaka huu peke yake, kwa sababu kwa miaka mingineyo yote ile tarehe ya uchaguzi imeweza kukitwa katika katiba yenyewe ikiwa ni siku ya Jumanne ya kwanza ya mwezi wa nane kila miaka mitano baada ya uchaguzi“.
Maoni ya walio wengi yanaonesha kupendelea kufanyika kwa uchaguzi mwezi wa Disemba mwaka huu kama ilivyopendekezwa na Odinga, wakitaka kuwaondowa madarakani haraka iwezekanavyo wabunge wabadhirifu, wavivu na wasiowajibika. Wakenya walio wengi wanahisi kwamba wabunge wa Kenya ambao hulipwa pesa nyingi, lakini wana mchango mdogo katika kuindeleza nchi.
Kenya bado yaugua
Kuhusiana na tetesi kwamba Raila Odinga huenda akajitoa katika chama chake,ili kutoa nafasi ya kuvunjika kwa serikali ya sasa na uchaguzi wa mapema kufanyika, wataalamu wanahisi kwamba si jambo linalowezekana.
Akinukuliwa na Barack Muluka, Odinga alisema “taifa hili (Kenya) bado linaugua kutokana na yale yaliyotokea miaka minne iliyopita, na halistahili kwa vyovyote vile kwenda katika uchaguzi ambao utakuwa umejikita katika muktadha wa malumbano na mambo ya majadiliano makali makali ya aina hii.
Wakati mahakama ikisubiriwa kutoa maamuzi yake juu ya rufaa ya kupinga tarehe ya uchaguzi, kuna khofu kwamba huenda mahakama hiyo ikatoa maamuzi yake kwa kuegemea upande mmoja wa serikali. Mahakama Kuu nchini Kenya iliwashangaza wengi pale ilipoamua kwamba uchaguzi utafanyika mwezi wa March mwakani na si Agosti kama ilivyoelekezwa na katiba.
Mwandishi: Hamad Omar Hamad
Mhariri: Mohammed AbdulRahman