1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani DRC waanzisha kampeni ya "Kwaheri Kabila"

Caro Robi
23 Novemba 2016

Zaidi ya vyama kumi vya upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo vimeungana kuanzisha kampeni ya kumshinikiza Rais Joseph Kabila kuondoka baada ya muda wake kukamilika mnamo tarehe 20 Disemba.

https://p.dw.com/p/2T6pM
Angola | Ankunft des kongolesischen Präsidenten Joseph Kabila bei einem meeting der süd- und zentralafrikanischen Staaten in Angola
Picha: REUTERS/K. Katombe

Kampeni hiyo iliyopewa jina la "Kwaheri Kabila" inamtaka rais huyo anayeshutumiwa kwa kuchelewesha chaguzi, kuondoka madarakani bila ya masharti yoyote na kutangaza waziwazi kuwa hatong'angania madaraka.

Mmoja wa waandaaji wa kampeni hiyo, Merveille Gozo, aliwaambia waandishi wa habari hapo jana (Novemba 22) kuwa wamekusanyika kuwaarifu watu wa Congo na jumuiya ya kimataifa kuhusu kampeni hiyo.

Gozo amesema wanapanga kufanya maandamano ya amani kuanzia Ijumaa kuashiria ni muda kwa Kabila kuingia katika kumbukumbu za historia kwa kukabidhi madaraka.

Katiba ya Congo inamzuia Rais Kabila kugombea muhula mwingine, lakini muafaka wa kisiasa na baadhi ya vyama vya upinzani umempa nafasi ya kuhudumu hadi mwaka 2018 baada ya kuitisha uchaguzi.