UNICEF: Uhaba wa maji safi waathiri Wasudan Kusini milioni 5 | Matukio ya Afrika | DW | 23.12.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

UNICEF: Uhaba wa maji safi waathiri Wasudan Kusini milioni 5

Shirika la UNICEF limesema Sudan Kusini inakabiliwa na tatizo la uhaba wa maji safi ya kunywa na pia uhaba wa vyoo jambo ambalo huenda likasababisha mripuko wa maradhi ya hatari mwaka 2021.

UNICEF imeyaomba mashirika ya misaada ya kimataifa yachangie fedha za kusaidia kumaliza tatizo hilo Sudan Kusini. Ripoti ya UNICEF inaeleza kuwa asilimia 40 ya watu Sudan Kusini hawana maji safi ya kunywa huku asilimia 61 wakiwa hawana vyoo vya kujisaidia jambo ambalo huenda likasababisha mripuko wa maradhi ya hatari mwaka 2021.

''Watu hawana vyoo na hii ni changamoto kubwa. Inabidi tupunguze tatizo hilo kila mtu awe na choo na hii ni juhudi ya jumuiya kwa pamoja" Amesema Samuel Madul ambaye ni kaimu mkurugenzi wa mpango wa usafi unaojulika kama Wash.

Soma pia:

Naye Margret Emanuel mkurugenzi wa shirika linaloshughulika na usafi na afya ya wanawake la African Women Health anasema hili ni tatizo kubwa sana kwenye miji ya Mundri, Western Equatorial, Juba na katika tarafa ya Luri na Lemon Ghaba hakuna kabisa vyoo.

''Kinyesi kinapokua sehemu moja mvua ikinyesha inichukua chote kwenye mto na watu wataanza kunywa maji bila kujua. bila shaka watu watapata kipindupindu, homa ya tumbo na maradhi mengine.'' Amesema Margret Emanuel.

UNICEF yasema Sudan Kusini yaathiriwa na ukosefu wa maji safi

UNICEF yasema Sudan Kusini yaathiriwa na ukosefu wa maji safi

Bi Margret ameongeza kusema kuwa badhi ya maeneo sasa yana visima vya maji kupunguza tatizo hilo, lakini kina mama wana kazi ya kuamka mapema sana saa 9 usiku kwenda kuchota maji hayo ya kisima.

Madul amesema wanahitaji dola milioni 45.6 kwa mwaka 2021, lakini kwa sasa wanahitaji dola milioni 1.7 za dharura kutumika kuanzia mwezi Januari hadi Juni ili kupambana na tatizo hilo. Nimemuuliza afisa huyo iwapo wana matumaini ya kupata fedha hizo kutoka kwa wafadhili wa kimataifa.

''Tunawaomba wafadhili washirikiane na sisi katika janga hili kuhakikisha wanashughulikia masuala ya maji na ubora wa afya yanawafikia hata watoto wadogo. na huu ndio wito wetu.'' Amesema Madul.

Bi Margret Samuel ambaye shirika lake la African Women Health linashughulikia masuala hayo ya usafi ameyataka mashirika ya kijamia yashirikianena na serikali ili kulimaliza tatizo hilo, la sivyo hali itakua mbaya sana.