1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yataka mapigano yasitishwe mara moja Libya

Bruce Amani
9 Aprili 2019

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito wa kusitishwa mapigano maramoja nchini Libya, baada ya wanajeshi wa kamanda Khalifa Haftar kuushambulia uwanja pekee wa ndege unaofanya kazi mjini Tripoli.

https://p.dw.com/p/3GUaz
Libyen Kämpfe in Tripolis
Picha: picture-alliance/ZumaPress

Umoja wa Mataifa umesema maelfu ya watu wamekimbia machafuko katika mji mkuu Tripoli tangu Haftar alipoanzisha operesheni ya ghafla wiki iliyopita ambayo imesababisha vifo vya watu kadhaa.

Taarifa ya Umoja wa Mataifa inasema Katibu Mkuu Guterres amezitaka pande zinazohasimiana kusitisha operesheni zao za kijeshi ili kupunguza mvutano na kuzuia kuzuka kwa mzozo mkubwa.

Ahmad al-Mesmari, msemaji wa jeshi la Haftar la Libyan National Army – LNA amesema kuwa shambulizi la jana kwenye uwanja wa ndege wa Mitiga, mashariki mwa Tripoli lililenga ndege ya MiG-23 na helikopta.

Bado hali sio shwari Libya

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya Ghassan Salame amesema shambulizi hilo linakiuka kabisa sheria ya kimataifa ambayo inakataza mashambulizi  dhidi ya miundombinu ya kiraia.

Msemaji wa shirika la ndege la Libya amesema mamlaka ya safari za anga nchini humo imesimamisha safari za ndege hadi muda usiojulikana.

Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa inadhibiti mji mkuu Tripoli, lakini mamlaka yake hayatambuliwi na serikali hasimu katika upande wa mashariki, inayoungwa mkono na Haftar.

Haftar akaidi miito ya kusitisha mashambulizi

Kamanda huyo amekaidi miito ya kimataifa ya kusitisha operesheni yake ya kuelekea Tripoli, ikiwa ni pamoja na kutoka kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Marekani.

Khalifa Haftar
Khalifa Haftar, kiongozi wa jeshi la LNA ameaviagiza vikosi vyake viiuchukuwe mji mkuu Tripoli.Picha: Getty Images/AFP/F. Monteforte

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini amezitaka pande zote nchini humo kusitisha shughuli zao za kijeshi na kurejea kwenye meza ya mazungumzo.

Serikali ya umoja wa kitaifa imesema kuwa Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amezungumza na kiongozi wake Fayez al-Sarraj ambapo alipinga vikali operesheni inayofanywa na vikosi vya Haftar.

Wizara ya afya ya serikali ya umoja wa kitaifa imesema jana kuwa idadi ya waliouawa imefika watu 35. Wanajeshi wa Haftar wamesema wapiganaji wao 14 wameuawa.

Umoja wa Mataifa umesema mapigano hayo yamesababisha watu 3,400 kuypoteza makaazi yao, tofauti na idadi ya awali iliyokadiriwa kuwa watu 2,800.