1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yashinikizwa kuandaa katiba ya Syria

Lilian Mtono
28 Septemba 2018

Marekani kwa ushirikiano na mataifa mengine sita ya Kiarabu na Ulaya yameutaka Umoja wa Mataifa hii leo kuchukua hatua ya dharura ya kuunda kamati itakayoandaa katiba ya baada ya vita nchini Syria.

https://p.dw.com/p/35d9Q
Schweiz UN Friedensgespräche für Syrien
Picha: picture-alliance/Photoshot/Xu Jinquan

Marekani kwa ushirikiano na mataifa mengine sita ya Kiarabu na Ulaya yameutaka Umoja wa Mataifa hii leo kuchukua hatua ya dharura ya kuunda kamati itakayoandaa katiba ya baada ya vita nchini Syria na kutoa taarifa kuhusu hatua watakayokuwa wameifikia ifikapo Oktoba 31.

Mawaziri wa mambo ya kigeni kutoka mataifa saba walikutana pembezoni mwa kikao cha baraza kuu la Umoja wa Mataifa ili kujadiliana kuhusu hatua za kuendeleza mchakato wa kisiasa nchini Syria, inayokabiliwa na vita kwa mwaka wa nane sasa.

Kwenye taarifa yao ya pamoja, wameunga mkono hatua ya dharura ya kuanzishwa kwa kamati na mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Syria, Staffan de Mistura, ambayo itaanza kazi ya kuandaa katiba mpya na kuweka msingi wa chaguzi.

Mataifa hayo saba, yamemuomba de Mistura kuliarifu baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hatua atakayokuwa amefikia kabla ya Oktoba 31, na kuweka muda wa mwisho wa utekelezaji, hii ikiwa ni kulingana na taarifa ya pamoja ya mataifa hayo.

Syrien Idlib Luftangriffe der Regierungskoaliltion
Raia wa Idlib nchini Syria, akiwa amesimama pembeni mwa nyumba yake iliyoharibiwa na bomu.Picha: Getty Images/AFP/O.H. Kadour

Kwenye kikao cha juu kilichojadili hali nchini Syria kilichofanyika juzi, De Mistura alikaribisha makubaliano yaliyofikiwa na Urusi na Uturuki kuhusu Idlib, na kuongeza kwa kuwa mashambulizi yalisitishwa dhidi ya jimbo hilo, sasa ulikuwa ni wakati wa hatua hiyo ya kisiasa ya kamati ya katiba ya Syria kuendelezwa.

Umoja wa Mataifa wasema, Wasyria sasa wana matumaini na hatua hiyo ya kisiasa.

De Mistura alinukuliwa akisema "Kwa kweli, marafiki zangu, watu wa Syria wana haki ya kutarajia hilo na kwa wakati huu. Na hakuna shaka kabisa kwamba ikiwa mchakato huo ulikuwa unaendelea na ulikuwa unatoa matokeo makubwa, utasaidia kuleta ufumbuzi wa mambo mengi. Ndiyo maana kila mtu atatazamia kuona kama kamati hii ya kikatiba inaweza kukutana  mwezi Oktoba, si wakati wa Krismasi na sio mwaka ujao.... mwezi Oktoba," alisisitiza

Misri, Ujerumani, Jordan na Uingereza wameungana na Marekani, Ufaransa na Saudi Arabia kuonya kwamba wale wanaotaka suluhu ya kijeshi watafanikisha tu kuongeza hatari zaidi ya kusambaa kwa machafuko.

Wanadiplomasia wa Magharibi wamesema makubaliano ya hivi karibuni na Urusi na Uturuki ya kuepusha mashambulizi ya kijeshi katika eneo hilo la Idlib ambalo ni ngome ya mwisho ya waasi nchini Syria, yametengeneza fursa ya kuanzishwa kwa mazungumzo ya kisiasa.

De Mistura aliliambia baraza hilo la usalama la Umoja wa Mataifa mwezi huu kwamba kulikuwa na mzozo uliokuwa ukiendelea kati ya serikali ya Syria na upinzani juu ya wajumbe wa kamati hiyo, ambayo awali ilitangazwa kwenye mkutano wa kilele uliofanyika nchini Urusi mwezi Januari.

Mjumbe huyo alisema anatarajia kwamba kamati hiyo huenda itaanza kazi katika wiki chache zijazo. Zaidi ya Wasyria 360,000, wamekufa kwenye vita hivyo vya miaka nane sasa, na mamilioni wamekimbia makazi yao.

Mwandishi: Lilian Mtono/AFPE/APE

Mhariri: Mohammed Khelef