1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yakaribisha miito ya kurejeshwa mazungumzo Libya

Bruce Amani
8 Juni 2020

Umoja wa Mataifa umesema umetiwa moyo na miito ya kurejeshwa mazungumzo ya kumaliza mzozo nchini Libya, siku moja baada ya Misri kutangaza mpango wa amani wa upande mmoja ukiungwa mkono na serikali ya upande wa mashariki

https://p.dw.com/p/3dPjh
Libyen-Ägypten-Waffenruhe
Picha: Getty Images/AFP/M. Turkia

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya umesema mapigano ya kuukamata mji mkuu Tripoli, kwa zaidi ya mwaka mmoja yamedhihirisha wazi kuwa vita yoyote miongoni mwa Walibya haitafanikiwa.

Taarifa hiyo imezihimiza pande zinazohasimiana Libya kushirikiana haraka katika mazungumzo ya kijeshi yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa kwa lengo la kufikia makubaliano ya kudumu ya kuweka chini silaha, yakifuatiwa na utekelezaji wa marufuku iliyowekwa upya na Umoja wa Mataifa ya Biashara ya Silaha.

Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sissi Jumamosi alitangaza mpango wa kumaliza vita, akisema unajumuisha usitishwaji wa mapigano kuanzia leo Jumatatu, kwa lengo la kusafisha njia ya kufanyika uchaguzi "Mpango huu pia unahakikisha uwakilishi wa haki wa maeneo yote matatu ya Libya katika baraza la rais, litakalochaguliwa na watu wa Libya chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa, ili wote waiongoze Libya kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hiyo."

Libyscher Militärbefehlshaber Khalifa Haftar mit dem ägyptischen Präsidenten Abdel Fattah al-Sisi im Präsidentenpalast in Kairo
Jenerali Khalifa na Rais al-Sissi wa Misri mjini CairoPicha: Reuters

Aliuzindua mpango huo mbele ya Kamanda Haftar ambaye anaungwa mkono na Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu na Urusi.

akizungumzia tamko la Cairo, Mohamad Gnounou, msemaji wa jeshi la serikali ya umoja wa kitaifa - GNA, alisema wao watachagua muda na mahali ambako vita hiyo itamalizikia.

Mpango wa Misri wa kumaliza mapigano ulikuja wakati vikosi vya Haftar vikipata hasara kubwa katika upande wa magharibi mwa Libya katika wiki za karibuni.

Wapiganaji watiifu kwa serikali ya Libya inayotambulika na Umoja wa Mataifa jana waliendeleza mashambulizi yao dhidi ya vikosi vya Haftar, lakini mapambano yamekwama viungani vya mji muhimu wa Sirte. Wanaungwa mkono na Uturuki, Qatar na Italia.

Sirte, mji wa pwani wa Mediterenia – nyumbani kwa dikteta wa zamani Muammar Gaddafi aliyeondolewa na kuuawa 2011 kupitia vuguvugu la mapinduzi likiungwa mkono na NATO – pia ni lango muhimu la visima vikubwa vya mafuta mashariki mwa nchi hiyo. Ambavyo bado vinadhibitiwa na vikosi vinavyomuunga mkono Haftar. Serikali ya umoja wa kitaifa –GNA inayoungwa mkono na Uturuki yenye makao yake mjini Tripoli, katika wiki za karibuni imeyakomboa ameneo yote yaliyobaki ya magharibi mwa Libya kutoka kwa wapiganaji wa Haftar.

Mjini Tripoli, umati wa watu ulisherehekea kurudi nyuma kwa vikosi vya Haftar, huku wakaazi wakionyesha alama ya ushindi na kupeperusha bendera ya taifa kwenye msafara wa magari yakipiga honi.