1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yahimiza pande hasimu Libya kutanguliza maslahi ya nchi

Sylvia Mwehozi
13 Oktoba 2020

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Libya Stephanie Williams amezihimiza pande hasimu nchini humo kutanguliza maslahi ya taifa badala ya kuweka mbele matamanio ya kisiasa wakati wa mazungumzo ya mwezi ujao.

https://p.dw.com/p/3jpzt
Libyen | Premierminister Rückttritt Fayiz as-Sarradsch
Picha: Media Office of the Prime Minister/Handout/Reuters

Taifa hilo la Afrika Kaskazini limetawaliwa na makundi yenye silaha yanayochochewa na mizozo ya ndani na mgawanyiko baina ya tawala mbili zinazopingana vikali, moja inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa iliyoko mjini Tripoli na ile ya Mashariki inayoongozwa na mbabe wa kivita Khalifa Haftar.

Nchi jirani ya Tunisia ndiyo itakuwa mwenyeji wa mazungumzo hayo yanayotarajiwa kufanyika mwanzoni mwa mwezi Novemba na kuwashirikisha wawakilishi kutoka asasi za kiraia, viongozi wa kikabila, viongozi wa kisiasa na wajumbe kutoka serikali zote mbili.

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya Stephanie Williams alikutana na rais wa Tunisia Kais Saied na kusema kuwa kinachotarajiwa katika mazungumzo hayo ni  wajumbe kuweka mbele maslahi ya nchi kabla ya jambo lolote. Alipoulizwa ikiwa Haftar au kiongozi wa serikali ya umoja wa Kiataifa Fayez al-Sarraj watashiriki mazungumzo hayo, mjumbe huyo alisema washiriki watahudhuria mkutano huo kwa sharti la "kwamba wanajiondoa kuzingatia nafasi za juu za serikali".

"Ninaweka sharti kwa yeyote kushiriki katika mazungumzo haya kwamba ajiondoe katika kuzingatia nafasi za juu za serikali. Hiyo ni pamoja na baraza la rais, uwaziri mkuu, mawaziri na nafasi za juu. Watu watakaokuwepo watawakilisha watu tofauti wa Libya," alisema mjumbe huyo. 

Libyen | Truppen von General Chalifa Haftar
Askari wa kikosi cha Khalifa HaftarPicha: Esam Omran Al-Fetori/Reuters

Mazungumzo hayo yanalenga kufanya maandalizi ya uchaguzi wa kitaifa. Waziri wa mambo ya kigeni wa Tunisia, Othman Jerandi ameyaita "mazungumzo kati ya walibya kuwa yanayoweza kuchangia upatikanaji wa suluhisho la kisiasa katika mgogoro huo".

Naye rais wa Tunisia Kais Saied alizungumza na mwenzake wa Algeria Abdelmadjid Tebboune, ambaye amesifu juhudi hizo mpya za mazungumzo na kusema Algeria ambayo pia ni jirani na Libya iko upande wa Tunisia.

Makubaliano ya awali baina ya pande hasimu za Libya, yalisainiwa nchini Morocco mwaka 2015 na ndiyo yaliunda serikali ya Umoja wa kitaifa ambayo haikuwa ikitambulliwa na Haftar.

Mwezi Aprili mwaka 2019, kamanda huyo alianzisha mashambulizi makali ya kuutwaa mji wa Tripoli, lakini alirejeshwa nyuma baada ya mwaka mmoja wa mapigano.

Tangu vikosi vyake vifurushwe magharibi mwa Libya, pande hizo mbili zimeanza tena mazungumzo yaliyo na ajenda maalumu zinazohusu taasisi, jeshi na masuala ya kisiasa. Mazungumzo ya mjini Tunis yanatarajiwa kuanza oktoba 26 kwa njia ya vidio kabla ya kuendelea ana kwa ana mwanzoni mwa mwezi Novemba.