UN: Kupunguzwa misaada kumesababisha mateso kwa wakimbizi
15 Desemba 2025
Wakimbizi wanaonekana kupuuzwa huku mateso yao yakitumiwa vibaya na magenge haramu na wanasiasa. Hayo yamesemwa hivi leo na Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi anayemaliza muda wake Filippo Grandi aliyeitaja hatua hiyo kuwa ya kutowajibika na kusisitiza kuwa mwaka huu umeshuhudia wimbi la migogoro iliyowalazimisha watu wengi kuyahama makazi yao, idadi iliyokadiriwa kuwa watu milioni 117.3 katikati ya mwaka huu wa 2025.
Aidha Grandi, amelaani "ukatili usio na kikomo" unaofanywa katika nchi za Sudan, Ukraine, Myanmar na huko Gaza, na kwamba kitendo cha kupunguzwa misaada ya kimataifa kimewasababishia wakimbizi madhila yasiyo ya lazima , hasa wakati huu ambapo idadi ya watu waliolazimika kuyahama makazi yao duniani kote imeongezeka mara mbili katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.