1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa wataka Sudan Kusini kufanya uchaguzi

18 Aprili 2024

Umoja wa Mataifa umevitaka vyama vyote vya siasa nchini Sudan Kusini kuchukua hatua za haraka ili kuruhusu uchaguzi uliocheleweshwa kwa muda mrefu unafanyika mwishoni mwa mwaka.

https://p.dw.com/p/4evC7
Rais Salva Kiir Mayardit wa Sudan Kusini.
Rais Salva Kiir Mayardit wa Sudan Kusini.Picha: Brian Inganga/AP Photo/picture alliance

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitoa ripoti inayoeleza kwamba ni muhimu vyama vyote vya siasa nchini Sudan Kusini "kuchukua hatua za dharura katika kufanikisha mchakato wa uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika."

Tarifa hiyo ya Guterres iliendelea kusema kuwa baada ya tathmini ya hali jumla, "Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) umehitimisha kuwa wadau wote bado wanahitaji msaada wa haraka katika masuala ya utaalamu, sheria na uendeshaji kwa ajili ya kuandaa uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Desemba mwaka huu au baadaye."

Soma zaidi: Juhudi za amani Sudan Kusini zasambaratika tena

Guterres alisema kumekuwa na ucheleweshaji wa shughuli na masharti muhimu yanayohitajika kabla ya kufanyika uchaguzi na kusisitiza kwamba itakuwa changamoto kubwa kwa taifa hilo masikini kuandaa kwa siku moja uchaguzi wa kitaifa, wa majimbo na serikali za mitaa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres.Picha: Yuki Iwamura/AP Photo/picture alliance

Tume ya taifa ya uchaguzi nchini humo ilitangaza wiki iliyopita shughuli za kuwaandikisha wapiga kura ingelianza mnamo mwezi Juni.

Lakini Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alisema yapo mengi yaliyocheleweshwa ikiwa ni pamoja na sensa ya kitaifa, kuandikwa kwa katiba ya nchi, na mchakato wa kuwarejesha makwao waliokimbia makaazi yao.

Aidha Guterres alisema viongozi wa Sudan Kusini wameafiki kwamba kuenea kwa ghasia katika baadhi ya maeneo madogo nchini humo kunaleta changamoto katika uendeshaji wa uchaguzi.

Hakujafanyika uchaguzi zaidi ya muongo mmoja

Sudan Kusini haijafanya uchaguzi tangu ilipojinyakulia uhuru wake kutoka Sudan mwaka 2011, na taifa hilo limekuwa likikumbwa na mizozo ya kila mara, umaskini uliokithiri na majanga ya asili.

Mipango ya uchaguzi imevurugwa na mabishano makali baina ya Rais Salva Kiir na mpinzani wake mkuu, Riek Machar, ambaye kwa sasa ndiye makamu wa rais.

Papa Francis aendeleza wito wa amani Sudan Kusini

Vikosi vinavyowatii wapinzani hao wawili vilipigana vita vya kikatili vya wenyewe kwa wenyewe kati ya mwaka 2013 hadi 2018, ambavyo vilisababisha vifo vya takribani watu 400,000 na kupelekea mamilioni ya wengine kuyakimbia makaazi yao.

Soma zaidi: Marekani, Uingereza zataka uchaguzi huru Sudan Kusini

"Vita vilikuwa vya kutisha mno. Watoto hawajapona majeraha ya kile walichopitia, na sasa tunajaribu kuwafanya wasahau walichopitia." Alisema Safa Abdulmutalleb, ambaye ni miongoni mwa wale wenye kumbukumbu mbaya ya vita hivyo vya kikatili.

Mkataba wa amani ulisainiwa mnamo mwaka 2018 na kuanzishwa kipindi cha mpito ili kuandaa mchakato wa kufanyika uchaguzi mkuu.

Lakini waangalizi wa kimataifa wana mashaka ya kutoheshimiwa kalenda ya uchaguzi wa Desemba, kwani Kiir na Machar bado hawajafikia muafaka wa namna ya kuandaa uchaguzi huo, au hata kujadili kuhusu nafasi zitakazogombaniwa.

Mapema wiki hii, Marekani ilisema kuwa viongozi wa kisiasa nchini Sudan Kusini walikuwa wameshindwa kufikia viwango vinavyohitajika ili kuandaa uchaguzi wa haki na wa amani unaotarajiwa kufanyika Desemba mwaka huu.