Umoja wa Mataifa waijadili Mashariki ya Kati | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.10.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Umoja wa Mataifa waijadili Mashariki ya Kati

Afisa wa Umoja wa Mataifa ameonya katika kikao cha dharura cha Baraza la usalama la Umoja huo jana (29.10.2014) mipango ya Israel kujenga makazi Jerusalem Mashariki inatishia uwezekano wa kuundwa taifa huru la Palestina.

Baraza la usalama lilikutana kufuatia ombi lililowasilishwa na mwanachama wa Jordan kwa niaba ya Wapalestina, wanaosisitiza juhudi za kujenga makazi ya wayahudi Jerusalem Mashariki zikome. Hali ya wasiwasi umeibuka tena kati ya waarabu na wayahudi kuhsiana na miapango ya Israel kujenga makazi 1000 katika eneo hilo, sehemu ambayo Wapalestina wanadai taifa lao la baadaye.

Mkuu wa masuala ya siasa wa Umoja wa Mataifa Jeffrey Feltman amesema kama makazi hayo yatajengwa yataibua tashwishwi kubwa kuhusu mipango ya Israel kutafua amani ya kudumu na Wapalestina, hususan wakati huu ambapo vidonda vilivyosababishwa na vita vya hivi karibuni katika Ukanda wa Gaza vinaendelea kupona.

Akikihutubia kikao cha dharura cha baraza la usalama Feltaman amesema, "Ukweli ni kwamba kuendelea na ujenzi wa makazi katika maeneo yanayokaliwa ya Palestina kunavuruga uwezekano wowote wa kupatikana amani ya kudumu kati ya pande mbili zinazohusika na kuisogeza hali karibu na ukweli wa kupatikana suluhisho la taifa moja." Feltman amependekeza baraza la usalama lilishughulikie suala hilo na kuzishinikiza pande zote mbili zisuluhishe tofauti za kwa njia ya mazungumzo.

Balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa Ron Prosor amesema nchi yake inafanya kila linalowezekana kutuliza hali ya mambo, lakini balozi wa Palestina katika umoja huo Riyad Mansour, amesema Israel haitaki kusikiliza na ameieleza hali kuwa mbaya.

Gaza Palästina Riyad Mansour Botschafter UN

Riyad Mansour

Mansour ameliambia baraza la usalama, "Kama hatuwezi kuishawishi kwa pamoja nchi inayoyakalia maeneo yetu kuzungumza na sisi kumaliza hatua hiyo na kuruhusu uhuru wa dola la Palestina na hivyo kufanikisha makubaliano ya kimataifa ya suluhisho la matafa mawili, basi fursa ya suluhisho la mataifa mawili huenda lisiwepo tena kwetu."

Mansour aidha amesema, "Na hakuna wa kulaumiwa isipokuwa nchi inayoyakalia maeneo yetu kwa kutochukua hatua kwa njia ya kuwajibika, kufanya mazungumzo na sisi kwa nia njema, kuacha kuyakalia maeneo yetu."

Marekani imeieleza mipango ya Israel ya kujenga makazi mapya kuwa ya kutia wasiwasi ikisema ujenzi wowote wa makazi utachochea zaidi wasiwasi uliopo.

Mpalestina auwawa Jerusalem Mashariki

Nchini Israel kwenyewe kikosi maalumu cha kupambana na ugaidi kimempiga risasi na kumuua mwanamume wa Kipalestina aliyeshukiwa kupanga njama ya kumuua mwanaharakati mashuhuri wa kiyahudi mwenye msimamo mkali. Kikosi hicho kiliizingira nyumba ya mshukiwa katika kitongoji cha Abu Tur huko Jerusalem Mashariki na kufyetua risasi wakati risasi zilipofyetuliwa kutokea ndani.

Rabbi Jehuda Glick Archivbild 2010

Rabbi Jehuda Glick, aliyepigwa risasi

Saa chache kabla mwanamume aliyekuwa kwenye pikipiki alimpiga risasi na kumjeruhi vibaya mwanaharakati wa kiyahudi Yehuda Glick mwenye umri wa miaka 48 anayeuongoza wakfu wa Temple Mount Heritage, unaowahimiza wayahudi kuhiji mahala hapo.

Sweden yalitambua taifa la Palestina

Wakati huo huo, Sweden leo imelitambua rasmi taifa la Palestina, wiki kadhaa tangu serikali ilipotangaza nia yake ya kuchukua hatua hiyo yenye utata. "Leo serikali inachukua uamuzi wa kulitambua dola la Palestina," amesema waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Sweden, Margot Wallstrom, katika taarifa iliyochapishwa katika gazeti la kila siku la Dagens Nyheter. Wallstrom amesema, "Ni hatua muhimu inayothibitisha haki ya Wapalestina kupigania uhuru wao."

Rais wa mamlaka ya ndani ya Wapalestina Mahmoud Abbas ameupongeza uamuzi huo wa Sweden akiuleza kuwa wa kishujaa na kihistoria. Sweden ni nchi ya kwanza ya Umoja wa Ulaya magharibi mwa bara la Ulaya kuitambua Palestina.

Mwandish: Josephat Charo/AFPE/APE

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com