Umoja wa Mataifa na mpango wa kusitisha mapigano Syria | Matukio ya Kisiasa | DW | 31.12.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Umoja wa Mataifa na mpango wa kusitisha mapigano Syria

Mpango wa Umoja wa mataifa wa kumaliza mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria kwa wito wa kuyaorodhesha makundi ya kigaidi yanayostahili kukabiliwa ni suala linaloendelea kuwaumisha vichwa wanadiplomasia

Kikao cha Baraza kuu la umoja wa Mataifa

Kikao cha Baraza kuu la umoja wa Mataifa

Mpango wa Umoja wa mataifa wa kumaliza mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliodumu karibu miaka mitano nchini Syria kwa wito wa kuyaorodhesha makundi ya kigaidi yanayostahili kukabiliwa ni suala linaloendelea kuwaumisha vichwa wanadiplomasia wanaojaribu kutanzua mgogoro katika taifa hilo la mashariki ya kati. Ambia Hirsi anaripoti

Hatua ya kukusitisha mapigano nchini Syria ilipitishwa na baraza kuu la umoja wa mataifa desemba 18 ikiyataka mataifa yenye nguvu duniani kama vile Marekani na Urusi,pamoja na washirika wao Iran na Uturuki lakini haiyahusishi makundi ya kigaidi ya dola la kiislamu linalofahamika pia kama ISIS na Nusra front lillilo na mafungamanao na al-Qaeda.

Wanadiplomasia wanasema matokeo yake huwenda yakawa ni nafuu , kwani itasaidia majeshi ya serikali na makundi ya waasi yanayokubalika, kutopigana risasi na badala kupam,bana na wapiganaji wa IS na makundi mengine yanayotajwa kuwa ya kigaidi.Jukumu la la kidiplomasia la kutambua makundi hayo ya kigaidi limepewa serikali ya Jordan.

Staffan de Mistura mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa

Staffan de Mistura mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa

Kwa upande mwengine katika kile kinacho onekana kuwa changamoto kwa usitishaji mapigano nchini Syria,kiongozi wa Kundi la waasi la Jeshi la Kiislamu aliuawa Ijumaa iliyopita katika shambulizi la angani ambalo duru za waasi hao zilisema lilifanywa na ndege ya Urusi. Kundi la waasi wa Jeshi la Kiislamu limekubali kushiriki mazungumzo ya kuleta amani.

Mapema wiki hii waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry alisema katika mazungumzo kwa njia ya simu na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov kwamba mauaji ya kiongozi wa kundi hilo yameleta utata katika juhudi za kutafuta muafaka wa kisiasa katika mzozo wa Syria.

Staffan De Mistura ambaye ni mjumbe wa tatu wa Umoja wa mataifa kutwikwa jukumu la kumaliza mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria ambayo yamesababisha vifo vya karibuwatu 250,000 na mamilioni ya wengine kulazimika kuhama makazi yao, amekuwa mstari wa mbele katika kutafuta mbinu tofauti zitakazo saidia kusitisha mapigano.

De Mistura anatarajiwa kuanzisha mazungumzo baina ya Rais wa Syria Bashar al-Assad na makundi pinzani mjini Geneva tarehe 25 Januari . Mazungumzo hayo yatajaribu kuzishawishi pande hizo mbili kukubaliana juu ya kipindi cha utawala wa mpito .

Mwandishi: Ambia Hirsi/RTRE

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com