1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya na vita dhidi ya uhamiaji

Saumu Mwasimba
24 Septemba 2018

Idadi rasmi ya waomba hifadhi walioko kwenye vituo vya kuwashikilia nchini Libya imefikia 5,000 lakini maelfu ya wengine zaidi inaaminika wameshikiliwa mateka katika maghala mengine kunakodaiwa kuna vitendo vya mateso.

https://p.dw.com/p/35PhB
Spanien hunderte Migranten haben den Grenzzaun von Ceuta erstürmt
Picha: Getty Images/A. Koerner

Idadi rasmi ya wanaoomba hifadhi na wakimbizi walioko kwenye vituo vya kuwashikilia nchini Libya imefikia 5,000, lakini maelfu ya wengine zaidi inaaminika wameshikiliwa mateka katika maghala na majengo mengine ambako kumekuweko ripoti zilizoenea zikisema kwamba kuna vitendo vya utumwa, unyanyasaji wa kingono na mateso mengine. Watalaamu na wadadisi wa mambo wanasema kwa hivyo suluhisho linalochukuliwa na nchi za Ulaya katika suala hili la wahamiaji linasababisha mgogoro wa kibinadamu. 

Mwezi huu wa Septemba, Umoja wa Mataifa ulivunja kimya chake kuhusu sera ya Umoja wa Ulaya ya kuruhusu walinzi wa pwani ya Libya  kuyawinda na kuyarudisha maboti ya wahamiaji wanaotumia bahari ya eneo hilo, ukisema  ni hatua isiyofaa na inayowaweka maelfu ya watu katika hatari ya kukamatwa na kufungwa maisha katika jela zizozokuwa na mazingira ya kiubinadamu hata kidogo.

Umoja wa Mataifa ulizungumzia yake madai ya kuwepo utesaji, ubakaji, matumizi ya nguvu pamoja na hali ya uonevu mkubwa unaofanyiwa watu wanapokuwa katika vizuizi vya kuwashikilia wakimbizi huko Libya. Umoja huo wa Mataifa kupitia shirika lake la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, unasema Libya katu haijafikia viwango vya kuitwa taifa salama.

Libyen Tripoli Flüchtlinge Sicherheitskräfte Razzia
Mwanajeshi wa Libya akiwalinda wahamiaji baada ya kuvamia eneo wanalilokuwa mwajificha nchini humo.Picha: Reuters/H. Amara

Pamoja na hayo ni kwamba takriban wakimbizi na waomba hifadhi wamesajiliwa na Umoja wa Mataifa nchini Libya na nchi jirani ya Niger nchi ambazo zote mbili zimepokea mamilioni ya Euro kwa kuridhia kutimiza ahadi ya Umoja wa Ulaya ya kuzitaka ziwachukue wahamiaji huku nchi hizo zikiahidi kuwatathmini baadhi ya wahamiaji ambao wataruhusiwa kuishi katika nchi hizo za Ulaya.

Hata hivyo kuna ukosoaji kwenye hatua hizo.

Lakini wanaokosoa mpango huo wanasema suala la kuwapa makaazi wahamiaji Ulaya halifanyiki. Kuna jumla ya watu 657 walioondoka Libya kwenda kupata makaazi Ulaya kufikia wiki iliyopita kati ya kundi la kwanza la watu 3,886 walioahidiwa katika kipindi cha zaidi ya mwaka 1 uliopita katika nchi 11 za Ulaya na Canada. Lakini wakati huo huo vituo vya kuwazuia wakimbizi nchini Libya na Ugiriki vinaendelea kufurika wahamiaji na wakimbizi wakisubiri kwa kipindi cha mwaka mzima au hata zaidi hadi pale uamuzi juu ya maombi yao utakapopitishwa.

Hiyo bila shaka ni hatua inayowafurahisha sana vyama vya kizalendo visivyopenda wageni barani Ulaya. Kimsingi mkimbizi yoyote atakayefanikiwa kufikia kisiwa cha Lesbos nchini Ugiriki amepiga hatua kubwa moja mbele kuliko yule aliyebakia Libya. Lakini pamoja na hilo hali hata huko Ugiriki ni mbaya kupita kiasi. Mitaro michafu iliyofurika ndiyo sura inayokupokea katika lango kuu la eneo la Moria ambako tatakata zimerundikana na kufanya mlima nje ya makontena ambako ndiko wanakolala wakimbizi.

Luka Fontana anafanya kazi na shirika la madaktari wasiokuwa na mipaka katika kisiwa cha Lesbos, Ugiriki, anasema robo ya watoto wenye umri mdogo wamekuwa wakijaribu kujiua wengine kila siku wanafikra za kujiua au kujidhuru. Hivi karibuni tu katika kontena moja huko Moria kundi kubwa la watoto waliokuwa hawana wazazi walijaribu kujikata mishipa ya damu kwa lengo la kutaka kufa.

Mwanasaikolojia Alessandra Barbero kutoka shirika hilo la madaktari wasiokuwa na mipaka anasema kambi ya Moria ni sehemu ambayo kwa hali ilivyo hapajawahi kuwa na eneo lenye muonekano kama huo Ulaya tangu katikati ya karne ya Ishirini. Na licha ya ukweli huu kilicho wazi ni kwamba matarajio ya kupatikana suluhisho rahisi katika suala hili lililoiacha Ulaya njia panda yamefifia.

Mwandishi: Saumu Mwasimba/AP

Mhariri: Mohammed Khelef