1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO yapania kuongeza nafasi yake Ulaya Mashariki

Saumu Mwasimba
29 Juni 2022

Viongozi wa jumuiya ya kijeshi ya NATO wakutana kwenye mkutano wa kilele mjini Madrid na lengo kubwa ni kuuimarisha muungano huo na nafasi yake Mashariki dhidi ya Urusi

https://p.dw.com/p/4DPTd
Spanien Nato-Gipfel Madrid
Picha: Bernd von Jutrczenka/dpa/picture alliance

Viongozi wa jumuiya ya kujihami ya NATO wameanza mkutano wao wa kilele,suala la vita nchini Ukraine likihodhi nafasi kubwa ya mazungumzo.

Mkutano wa kilele wa jumuiya ya kijeshi ya NATO unafanyika mjini Madrid nchini Uhispania na tayari viongozi wa Jumuiya hiyo wameshasema kwamba lengo kubwa la mkutano huo ni kuimarisha vikosi vya jumuiya hiyo katika ulaya Mashariki na kujenga uthabiti wa ulinzi dhidi ya Urusi.

Katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg amesema mkutano huu wa kilele ni wa kihistoria na utakaoleta mabadiliko katika mustakabali wa muungano huo.

NATO-Gipfel in Spanien
Picha: Henrik Montgomery/TT/AP/picture alliance

Rais Joe Biden wa Marekani amebaini NATO ni chombo Imara na  chenye mshikamano na mkutano huu unataka kuuongezea nguvu muungano huo. Jana usiku mfalme Phillipe wa Uhispania aliwakaribisha viongozi wote wa jumuiya hiyo waliofika kwenye dhifa maalum ya chakula na kutoa mwito maalum kuelekea mkutano huu na kusisitiza Jumuiya hiyo inapaswa kuiunga mkono Ukraine.

"Wale tunaoamini katika demokrasia,haki za binadamu na sheria za wazi zenye kuzingatia utaratibu wa kimataifa,wakati tumekusanyika hapa wakati huu,tunapaswa kusimama pamoja kuwaunga mkono watu wa Ukraine.Fikra zetu leo ziko pamoja na wananchi na viongozi wa taifa hilo jasiri ambao ushupavu na heshima zao zimetugusa sote.

Wakati akiwasili leo Jumatano kwenye mkutano huo waziri mkuu wa Uingereza  Boris Johnson alisema NATO inahitaji kupata funzo kutokana na miezi michache iliyopita na kuona haja ya kutathmini nafasi yake katika eneo la Mashariki mwa Ulaya.

Spanien I NATO Gipfel I Recep Tayyip Erdogan
Picha: Bernat Armangue/AP/picture alliance

Rais wa Poland Andrzej Duda kwa upande wake ameweka wazi kwamba anaamini kujitolea kwa NATO kuongeza haraka kikosi chake cha kuchukua hatua kuzilinda nchi wanachama zinazokaribiana na Urusi ni jambo litakaloifanya Ulaya kuwa salama.Rais huyo wa Poland amesema Urusi ni kitisho kwa Ulaya na sio tu Ulaya bali kwa wanachama wote wa jumuiya ya NATO.

NATO imeshasema kwamba itaimarisha kikosi chake cha kujibu mashambulizi ambacho sasa kinawanajeshi 40,000.Kikosi hicho kitaongezwa hadi kufikia wanajeshi laki tatu kwaajili ya kutoa ulinzi kwenye eneo la Ulaya mashariki linalojumuisha mipaka ya Poland na Ukraine na Belarus ambayo ni mshirika wa karibu wa Urusi.

Bundeswehr in Litauen
Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Mkutano uliofunguliwa leo umeanza kwa mazungumzo ya awali ambayo yatatuwama katika kutazama namna NATO inavyoweza kutoa msaada kwa Ukraine.Lakini pia viongozi wa Jumuiya hiyo wanajiandaa kuzikaribisha Finland na Sweden kujiunga na mfungamano huo baada ya Uturuki kuziondolea pingamizi.