1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaVenezuela

Ukosoaji waendelea, Maduro apandishwa kizimbani

5 Januari 2026

Kiongozi wa Venezuela Nicolas Maduro aliyetekwa wiki iliyopita na vikosi vya Marekani, anafikishwa Mahakamani Jumatatu mjini New York akituhumiwa makosa ya usafirishaji wa madawa ya kulevya.

https://p.dw.com/p/56KwJ
Marekani | Rais wa Venezuela Nicolás Maduro akiwa mikononi mwa maafisa wa DEA
Rais wa Venezuela Nicolas Maduro (kushoto) akiwa amekamatwa na maafisa wa Marekani wa kudhibiti madawa ya kulevya.Picha: REUTERS

Nicolas Maduro na mkewe wanakabiliwa na mashtaka ya kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya baada ya wawili hao kuvamiwa na makomandoo wa Marekani siku ya Jumamosi na kusafirishwa hadi Marekani ambapo hii leo watapandishwa kizimbani.

Awali, serikali ya Venezuela ilipinga vikali hatua hiyo ya Marekani na kutaja kuwa Maduro ndiye rais anayetambulika wa Venezuela. Trump  alijibu kwa kutoa vitisho kwa Makamu wa rais wa Venezuela Delcy Rodríguez kwa kusema kuwa endapo hatofanya maamuzi sahihi, basi "atalipa gharama kubwa zaidi" kuliko ile iliyomkuta Maduro.

Baadaye Delcy Rodriguez ambaye kwa sasa ndie kaimu rais alitangaza kuwa Venezuela iki tayari kushirikiana na Marekani kwa ajili ya "maendeleo ya pamoja" na kwamba serikali yake inatoa kipaumbele kwa hatua ya kuelekea uhusiano wa kuheshimiana na Marekani.

Wasiwasi na ukosoaji wa kimataifa

Venezuela imeitisha kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kitakachofanyika siku ya Jumatatu, na ambacho kitatumiwa kama jukwaa la kuelezea wasiwasi wa kimataifa kuhusu nia ya Marekani katika nchi hiyo yenye watu wapatao milioni 30.

Istanbul 2018 | Rais wa Venezuela Nicolas Maduro akiwa na mkewe Cilia Flores
Rais wa Venezuela Nicolas Maduro akiwa na mkewe Cilia Flores walipotembelea Uturuki mwaka 2018Picha: Orhan Akkanat/Anadolu Agency/IMAGO

Jumuiya ya kimataifa pia imeendelea kukosoa hatua ya Marekani kumteka kiongozi wa Venezuela. Umoja wa Afrika na ule wa Ulaya zimelezea 'wasiwasi mkubwa' kuhusu kukamatwa kwa Maduro, huku Urusi, China na Iran zikitoa wito wa kuachiliwa mara moja kwa Maduro na mkewe.

Lin Jian, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amesema kitendo hicho ni utekaji na kinakiuka sheria za kimataifa na kwamba China imeshtushwa mno na inalaani vikali matumizi ya nguvu ya Marekani dhidi ya taifa huru na kumdhibiti rais wake kwa nguvu.

Jian ameendelea kusema kuwa vitendo hivi vya kimabavu vinavyofanywa na Marekani vinakiuka sheria za kimataifa, vinakiuka uhuru wa  Venezuela , na vinatishia amani na usalama katika eneo la Amerika Kusini na Caribean.

"Tunaihimiza Marekani kufuata sheria za kimataifa na kuheshimu kanuni za Umoja wa Mataifa, na kuacha kukiuka uhuru na usalama wa nchi zingine, " alisisitiza afisa huyo wa serikali ya China.

China imechukizwa mno na kitendo cha Marekani cha kumuondoa rais wa Venezuela, nchi yenye mahusiano ya kimkakati na Beijing. Pia, maelfu ya raia wa Venezuela wameandamana kulaani kitendo cha rais wao kutekwa. Lakini licha ya yote hayo, Trump anaonekana kuendelea kuimarisha mpango wake wa kuitawala Venezuela na kuhodhi visima vyake vikubwa vya mafuta.