1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujumbe wa usalama wa Misri wafanya ziara nchini Libya

Saleh Mwanamilongo
28 Desemba 2020

Wanadiplomasia na maafisa wa ujasusi wa Misri wamekutana na maafisa wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya iliyoko mjini Tripoli.

https://p.dw.com/p/3nIBP
Waziri mkuu wa Libya Fayez al-Sarraj ( kushoto) na waziri wa ulinzi wa Uturuki Hulusi Akar, mjini Tripoli
Waziri mkuu wa Libya Fayez al-Sarraj ( kushoto) na waziri wa ulinzi wa Uturuki Hulusi Akar, mjini Tripoli.Picha: Getty Images/AFP

Wanadiplomasia na maafisa wa ujasusi wa Misri Jumapili wamekutana na maafisa wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya iliyoko mjini Tripoli, ikiwa ni ujumbe wa kwanza wa ngazi ya juu zaidi wa Misri kutembelea eneo la magharibi la nchi hiyo lililokumbwa na mizozo kwa miaka kadhaa. Wakati huo huo Uturuki imetahadharisha kuwa vikosi vya mbabe wa kivita mashariki ya Libya, Khalifa Haftar na wafuasi wake kwenye eneo hilo vitalengwa iwapo vitajaribu kuwashambulia wanajeshi wa Uturuki waliopo nchini libya. 

Waziri wa ulinzi wa Uturuki, Hulusi Akar amemuonya jenerali Khalifa Haftar kwamba, Uturuki itajibu shambulizi lolote dhidi ya wanajeshi wake walioko Libya.

 ''Mhalifu huyo wa kivita, Haftar na wafuasi wake wanatakiwa kufahamu kwamba ikiwa watajaribu kushambulia vikosi vya Uturuki, wapiganaji wa muuwaji Haftar watalengwa mahala popote walipo. Wanatakiwa kufahamu hilo katika vichwa vyao''.

Msimamo huo umefuatia kauli ya mbabe wa kivita wa mashariki mwa Libya Khalifa Haftar kuvitaka vikosi vyake kupambana na kuviondoa vikosi vya Uturuki vinavyoiunga mkono serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa.

Wakati huo huo, waziri wa mambo ya ndani wa serikali ya Tripoli, Fathi Bashagha amesema mazungumzo baina ya ujumbe wa Misri na serikali ya Libya, yalihusu changamoto za kiusalama na namna ya kuimarisha ushirikiano.

Pia walijadili njia za kuunga mkono makubaliano yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa ya kusitisha mapigano, ambayo yalitiwa saini na pande zinazohasimiana Libya mnamo mwezi Oktoba.

Misri kufungua upya Ubalozi wake mjini Tripoli

Türkische Soldaten in Libyen
Picha: MAHMUD TURKIA/AFP/Getty Images

Ziara hiyo ya maafisa wa Misri inafanyika siku moja baada ya maafisa wa Uturuki nao kuitembelea Tripoli. Ujumbe wa Misri uliongozwa na Ayman Badea, naibu mkuu wa idara ya upelelezi ya nchi hiyo.

Ujumbe huo ulikuwa pia na mashauriano na Emad Trapolsi, mkuu wa idara ya upelelezi na Ahmed Matiq, naibu waziri mkuu wa Libya. Matiq amesema pamoja na ujumbe wa Misri, walijadili uwezekano wa kufunguliwa upya ubalozi wa nchi hiyo mjini Tripoli ambao ulifungwa kwa zaidi ya miaka sita na vilevile kuanzishwa upya kwa usafiri wa ndege ya abiria baina ya Cairo na Tripoli.

Hapakuwa na taarifa yoyote upande wa Misri kufuatia ziara hiyo. Wizara ya mambo ya nje ya Misri haikujibu simu za shirika la habari la Associeted Press kwa ajili ya ziara hiyo.

Ziara hiyo ya ujumbe wa Misri mjini Tripoli, imefanyika wiki moja baada ya ile alioifanya mjini Benghazi, Abas Kamel, mkuu wa idara ya ujasusi ya Misri. Alikutana na mbabe wa kivita Khalifa Haftar na spika wa bunge la mashariki Aguila Saleh.

Fathi Bashagha, waziri wa mambo ya ndani wa serikali ya muungano wa kitaifa ya mjini Tripoli anatarajiwa kuongoza serikali ya kipindi cha mpito kwa ajili ya kuitisha uchaguzi mkuu wa Desemba mwaka ujao.

Libya imegawanyika katika serikali mbili, moja ikiwa Tripoli na nyingine Benghazi. Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu zinaunga mkono majeshi ya Mashariki yanayoongozwa na mbabe wa kivita Kamanda Khalifa Haftari wakati Uturuki ni mshirika wa serikali ya Tripoli.