Ujumbe wa Uingereza wakutana na maafisa wa Taliban | Matukio ya Kisiasa | DW | 05.10.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Ujumbe wa Uingereza wakutana na maafisa wa Taliban

Ujumbe kutoka Uingereza umeshiriki mazungumzo na wanachama wa serikali mpya ya Afghanistan ya Taliban wakati maafisa wa serikali hiyo wakisema baadhi ya wasichana wamerejea katika shule za upili Kaskazini mwa nchi hiyo.

Kulingana na ofisi ya masuala ya kigeni ya Uingereza, mwakilishi maalumu wa serikali Simon Gass amekutana na manaibu waziri wakuu Abdul Ghani Baradar na Abdul Salaam Hanafi, na wamejadili namna Uingereza inavyoweza kuisaidia Afghanistan kushughulikia tatizo la mgogoro wa kibinaadamu, ugaidi na umuhimu wa kuwepo njia salama kwa wale wanaotaka kuondoka nchi hiyo.

Msemaji wa serikali ya Uingereza amesema ujumbe huo pia uligusia namna watu wa jamii za wachache wanavyotendewa na pia kuhusu haki za wanawake na wasichana.

Amesema serikali ya Uingereza inaendelea kufanya kila iwezalo kuhakikisha uwepo wa njia hiyo salama na inajitolea kuwasaidia watu wa Afghanistan.

Abdul Qahar Balkhi msemaji wa wizara ya kigeni ya Taliban amesema mkutano huo ulijikita pia katika majadiliano mapana kuhusu ufufuaji wa uhusiano kati ya mataifa hayo mawili.

Wasichana waripotiwa kurejea shuleni

Afghanistan, Herat | Mädchen gehen wieder in die Schule

Wasichana wakiwa darasani Afghanistan

Huku hayo yakiarifiwa maafisa wa Taliban na walimu Afghanistan wamesema, baadhi ya wasichana wamerejea katika shule za upili Kaskazini mwa nchi hiyo.

Serikali mpya ya Afghanistan pia imetangaza kuwa baadhi ya wafanyakazi wa Umma wanawake wametakiwa kurejea kazini huku wakihakikishiwa mishahara yao, hii ikiwa ni ishara kuwa kundi hilo lililo na itikadi kali linajaribu kujisafisha na kubadili muonekano wake duniani baada ya kuwa madarakani kwa siku 50.

Vidio iliyotumwa na msemaji wa kundi hilo Suhail Shaheen, imewaonyesha wanafunzi kadhaa wakike waliovalia hijabu nyeusi na nyeupe  na wengine wakiwa wamefunika nyuso zao, wakiwa wamekaa vitini huku wakipeperusha bendera ya Taliban.

soma zaidi: Borrell: Sera za Taliban zinakwamisha msaada kwa Afghanistan

Shaheen aliyeteuliwa kama muakilishi wa kudumu wa serikali mpya ya Afghanistan katika Umoja wa Mataifa ameandika katika ujumbe wake wa twitter, kwamba  wasichana wanakwenda shuleni katika eneo la Khan Abad mkoa wa Kunduz.

Lakini mjini Kabul afisa katika wizara ya elimu  Mohammad Abid amesema bado hapajakuwa na mabadiliko yoyote ya sera kutoka kwa serikali ya mpito ya Taliban kwahiyo shule za sekondari bado zinaendelea kufungwa kwa wasichana hao.

Kundi hilo la Taliban linalojulikana kwa uongozi wake wa kikatili na ukandamizaji  kuanzia mwaka wa 1996 hadi mwaka 2001 limekumbwa na ukosoaji mkubwa kimataifa kutokana na hatua ya kuwabagua wanawake na wasichana kupata elimu, kufanya kazi  na kuwanyima uhuru wao.    

Chanzo: afp, reuters