1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaNicaragua

Ujerumani yajitetea katika mahakama ya ICJ

Tatu Karema
9 Aprili 2024

Mahakama ya kimataifa ya haki ICJ imeelezwa leo kwamba usalama wa Israel uko katika misingi ya sera ya mambo ya nje ya Ujerumani, katika kesi ambapo nchi hiyo inajitetea dhidi ya madai ya kuisaidia Israel kwa silaha

https://p.dw.com/p/4eZiB
Mwakilishi wa Ujerumani katika kesi kwenye mahakama ya ICJ Tania von Uslar-Gleichen (kushoto) akihudhuria kesi hiyo ya madai ya Nicaragua kwamba Ujerumani inaisaidia Israel kwa silaha
Wakili wa Ujerumani katika kesi kwenye mahakama ya ICJ - Tania von Uslar-Gleichen (kushoto)Picha: Dursun Aydemir/Anadolu/picture alliance

Wakili wa Ujerumani katika kesi hiyo inayosikilizwa katika mahakama ya ICJ Tania von Uslar-Gleichen, ameiambia mahakama hiyo kwamba historia ya nchi hiyo ndiyo sababu kuu ya kwanini usalama wa Israel unazingatiwa zaidi katika sera yake ya mambo ya nje.

Uslar-Gleichen, amesema kuwa nia ya msaada wa Ujerumani kwa Israel unaojumuisha silaha na vifaa vingine vya kijeshi,imetafsiriwa kimakosa na Nicaragua.

Ujerumani ina jukumu la kuikumbusha Israel kuhusu sheria ya kimataifa ya kibinadamu

Uslar-Gleichen amesema katika hali ambayo Israel inakabiliwa na mashambulizi yanayoendelea ya wanamgambo wa Hamas, ni jukumu la Ujerumani kuikumbusha kwamba hata inapotumia haki yake ya kujilinda, sheria ya kimataifa ya kibinadamu bado inatumika .

Soma pia: Nicaragua yaiomba Mahakama ya Haki ya Kimataifa kuiagiza Ujerumani kuacha kuiuzia silaha Israel

Ujerumani imeipinga vikali kesi iliyowasilishwa mbele ya mahakama hiyo ya kimataifa ya haki na Nicaragua, inayoituhumu kuisadia Israel kukiuka mikataba ya haki za binadamu ya kimataifa, kwa kuipatia nchi hiyo silaha na usaidizi wa aina nyingine katika vita vyake vya Gaza.

Jukumu la mataifa yalio chini ya Mkataba wa Mauaji ya Kimbari

Ujerumani na Israel ni nchi mbili kati ya zaidi ya 150 zinazoshiriki katika mkataba huo, pamoja na Nicaragua.

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akihudhuria mkutano wa baraza la mawaziri wa  kila wiki katika wizara ya ulinzi mjini Tel Aviv mnamo Januari 7, 2024
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu Picha: Ronen Zvulun/AFP/Getty Images

Hii inamaanisha kuwa kila taifa lililotia saini mkataba huo, lina jukumu la kisheria la kuzingatia masharti yake na kuwa na haki ya kulishtaki taifa lingine rasmi kwa ukiukaji wake.

Madai ya Nicaragua dhidi ya Ujerumani

Mnamo Machi 1, Nicaragua iliwasilisha kesi dhidi ya Ujerumani katika mahakama ya ICJ inayodai kuwa Ujerumani kwa msaada wake kwa Israel ikiwa ni pamoja na usambazaji wa silaha imeshindwa kutimiza majukumu yake ya kuzuia madai ya mauaji ya kimbari yaliofanyika na yanayofanyika dhidi ya raia wa Palestina na hivyo basi kuchangia kufanyika kwa mauaji hayo kwa kukiuka mkataba huo na vipengele vyengine vya sheria ya kimataifa.

Soma pia:Mahakama ya Haki yaanza kusikiliza kesi dhidi ya Ujerumani

Nicaragua  imeitaka ICJ, kuweka hatua za dharura kuizuia Ujerumani kutoa silaha zaidi kwa Israel pamoja na msaada mwingine.

Umoja wa Mataifa na mashirika ya kutetea haki za binadamu yamevishtumu vikosi vya Israel kwa mauaji ya kiholela dhidi ya raia. Mataifa washirika wa Israel kama Marekani pia wametaja idadi ya vifo vya raia kuwa  juu.