1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yahimiza uwajibikaji wa kimataifa ukanda wa Gaza

21 Novemba 2023

Annalena Baerbock ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua jukumu muhimu la kulinda raia katika ukanda wa Gaza baada ya mzozo wa sasa kati ya Israel na kundi la wanamgambo la Hamas kukakamilika.

https://p.dw.com/p/4ZErE
Berlin, ujerumani | Annalena Baerbock katika mahojiano na Jaafar Abdul Karim
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock katika mahojiano na mwandishi wa DW Jaffar Abdul KarimPicha: Ronka Oberhammer/DW

Akizungumza na mwandishi wa DW Jaafar Abdul-Karim, Baerbock amehimiza jamii ya kimataifa kufanya juhudi zaidi kupunguza mzozo kwa sasa.

Ametetea msimamo wa Ujerumani wa kuhimiza usitishwaji wa vita kwa muda mrefu, na kusisitiza kuwa kipaumbele kwa wakati huu kinapaswa kupeleka misaada ya kibinadamu kwa wakaazi wa Gaza.

Mwanadiplomasia huyo wa Ujerumani ameeleza kuwa, pindi tu mzozo wa sasa utakapokamilika, jamii ya kimataifa inapaswa kuhakikisha hali ya utulivu inarudi katika ukanda wa Gaza ndani ya muktadha wa suluhisho la mataifa mawili kwenye mzozo wa Israel na Palestina. Ameiambia DW kuwa, "ili kuhakikisha usalama, tunahitaji uwajibikaji wa kimataifa."

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani ameitembelea Israel mara tatu tangu mzozo ulipozuka mnamo Oktoba 7 wakati wanamgambo wa Hamas walipofanya shambulizi ndani ya ardhi ya Israel na kuua watu 1,200 na kuwachukua mateka watu 240.

Kama njia ya kulipiza kisasi, Israel ilianzisha mashambulizi ya anga na ardhini katika ukanda wa Gaza. Kwa mujibu wa wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas, zaidi ya watu 13,000 wameuawa huko Gaza.

Baerbock atetea msimamo wa Ujerumani

Berlin | Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan katika ziara nchini Ujerumani
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan (kushoto) na Kansela wa Ujerumani Olaf ScholzPicha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Akizungumza na mwandishi wa DW Jaafar Abdul-Karim, Baerbock ametetea msimamo wa Ujerumani wa kuhimiza usitishwaji wa vita kwa muda mrefu, na kusisitiza kuwa kipaumbele kwa wakati huu kinapaswa kuwa kupeleka misaada ya kibinadamu kwa wakaazi wa Gaza.

Mwanadiplomasia huyo wa Ujerumani ameeleza kuwa, pindi tu mzozo utakapokwisha, jamii ya kimataifa inapaswa kuhakikisha hali ya utulivu inarudi katika ukanda wa Gaza ndani ya muktadha wa suluhisho la mataifa mawili. Ameiambia DW "Ili kuhakikisha usalama, tunahitaji uwajibikaji wa kimataifa." 

Soma pia: UN: Wakimbizi wa Kipalestina wanaishi katika mazingira duni 

Kumetolewa miito kimataifa ya kusitisha kabisa mapigano huko Gaza. Hata hivyo, Ujerumani, Marekani na Umoja wa Ulaya badala yake zimeendelea kuhimiza wazo la usitishaji vita kwa muda tu ili kuruhusu misaada ya kibinadamu kufikishwa Gaza, wakihoji kuwa usitishwaji vita kabisa kutalipa muda kundi la Hamas kujipanga upya.

Guterres alaani mauaji ya raia hasa watoto

USA New York | Baraza la Usalama la UN | Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: Seth Wenig/AP Photo/picture alliance

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali mauaji ya raia hasa watoto katika mashambulizi yanayoendelea huko Gaza.

Guterres amewaambia waandishi wa habari kuwa, bila ya kuingia kwenye mjadala juu ya idadi kamili ya wahanga iliyochapishwa na mamlaka huko Gaza, kilicho wazi ni kwamba maelfu ya watoto wameuawa katika muda wa wiki chache tu.

Ameongeza kuwa, anashuhudia mauaji ya raia ambayo hayajawahi kutokea katika mzozo wowote tangu alipochukua nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Soma pia: WHO kuanzisha hospitali katika Ukanda wa Gaza 

Wakati hayo yakiarifiwa, wizara ya afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas imesema kuwa wagonjwa 100 wamehamishwa kutoka hospitali iliyojengwa kwa msaada wa serikali ya Indonesia. Wagonjwa hao walihamishwa kwa usaidizi wa shirika la kimataifa la hilali nyekundu na msalaba mwekundu ICRC baada ya hospitali hiyo kushambuliwa na makombora ya Israel.

Msemaji wa wizara ya afya Ashraf al-Qudra ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, wagonjwa wengine 100 pia watahamishwa na kupelekwa katika kituo kingine cha matibabu katika mji wa kusini wa Khan Yunis.