Ujerumani, Ufaransa zatoa msimamo wa pamoja | Matukio ya Kisiasa | DW | 31.05.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Ujerumani, Ufaransa zatoa msimamo wa pamoja

Viongozi wa Ujerumani na Ufaransa wameufungua ukurasa mpya baada ya miezi kadhaa ya mvutano kuhusu namna ya kuukabili mzozo wa kanda ya sarafu ya euro. Hii inafuatia ziara ya Kansela Angela Merkel Paris

France's President Francois Hollande (R) and German Chancellor Angela Merkel attend a joint news conference at the Elysee Palace in Paris, May 30, 2013. REUTERS/Charles Platiau (FRANCE - Tags: POLITICS)

Francois Hollande Angela Merkel

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Rais wa Ufaransa Francois Hollande wametoa mapendekezo ya pamoja kuhusu ushindani, ukuaji, nafasi za kazi na ushirikiano wa karibu wa kiuchumi na kifedha.

Waziri wa fedha wa Uholanzi Jeroen Dijsselbloem anahudumu kama mwenyekiti mawaziri wa fedha wa kundi la euro

Waziri wa fedha wa Uholanzi Jeroen Dijsselbloem ndiye mwenyekiti mawaziri wa fedha wa kundi la euro

Rais wa Ufaransa Francois Hollande amewaambia waandishi wa habari mjini Paris, akiwa na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, kuwa hali huwa ile ile wakati watu wanapozungumza kuhusu Ufaransa na Ujerumani. Wanafikiri kuwa nchi hizo mbili hazikubaliani, na ilhali mara nyingi wao hukubaliana. Hollande amekuwa akitaka makubaliano mapana kuhusu uchumi unaoyumbayumba katika kanda ya sarafu ya euro, wakati Merkel akizitaka serikali zinazokabiliwa na matatizo ya kifedha kwanza ziziweke sawa hali zao za bajeti.

Hollande na Merkel wazungumza sauti moja

Hapo jana, hata hivyo, viongozi hao wawili walikuwa na msimamo wa pamoja wakati walipowasilisha mapendekezo ya pamoa kuhusu namna ya kuikwamua kanda ya sarafu ya euro kutoka lindi la mgogoro. Waraka huo kwa jina "Ufaransa na Ujerumani - Pamoja kwa Ulaya yenye nguvu za uimara na ustawi" utawasilishwa kwa viongozi wengine wa Umoja wa Ulaya katika mkutano wa kilele mnamo Juni 27 na 28.

Kiwango cha ukosefu wa ajira barani Ulaya kimeongezeka hasa Uhispania na Ufaransa

Kiwango cha ukosefu wa ajira barani Ulaya kimeongezeka hasa Uhispania na Ufaransa

Ufaransa na Ujerumani zinataka kundi la mwaziri wa fedha wa kanda ya sarafu ya euro, ambao kwa sasa wanaongozwa na Waziri wa fedha wa Uholanzi Jeroen Dijsselbloem, likuwe na rais atakayehudumu muhula mzima na pia viongozi 17 wa kanda ya sarafu ya euro wakutane mara kwa mara.

Nchi hizo mbili jirani pia zimeweka mipango ya kutatua mzozo wa ukosefu wa ajira barani ulaya. Takwimu mpya za kiwango cha ukosefu wa kazi zilizotolewa jana Ufaransa, zimeonesha kuwa watu 40,000 walikosa kazi mwezi Aprili na kufikisha milioni 3.27 idadi ya Wafaransa wasio na kazi.

Miongoni mwa mapendekezo yaliyomo kwenye muafaka huo wa ushirikiano kati ya Ufaransa na Ujerumani ni: utekelezwaji wa haraka wa mpango wa ajira kwa vijana wa euro bilioni 6, ambao unapatikana katika bajeti ya Umoja wa Ulaya ya 2014-2020. Kuwaunga mkono vijana wa Ulaya kumalizia masomo yao katika nchi nyingine ya Umoja wa Ulaya, na kuikubalia Benki ya Mandeleo ya Ulaya kufadhili bishara ndogondogo na za wastani, ambazo zitabuni nafasi za kazi. Umoja wa Ulaya siku ya Jumatano ulitoa wito kwa Ufaransa, ambayo ni nchi ya pili kwa ukubwa kiuchumi, kufanya mageuzi ya dharura, ikiwa ni pamoja na soko lake la ajira na mfumo wa pensheni.

Mwandishi: Bruce Amani

Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com