1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani: Tutaisaidia kifedha WHO

Babu Abdalla25 Juni 2020

Shirika la afya duniani limepigwa jeki katika vita vyake dhidi ya virusi vya Corona baada ya Ufaransa na Ujerumani kusema zitalisaidia shirika hilo kifedha na kisiasa.

https://p.dw.com/p/3eKom
EU-Gipfel | EU-Wahlen | Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Reuters/P. van de Wouw

Ujerumani imesema itatoa ufadhili wa kiasi cha euro milioni 500 kwa WHO mwaka huu.

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi habari mjini Geneva, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya duniani Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema kuwa shirika hilo linaendelea kupata ufadhili unaohitajika wa kifedha na wa kisiasa.

Tangazo la Ufaransa na Ujerumani la kusema zitalisaidia shirika hilo kifedha linakuja baada ya Marekani kulilibesha lawama kwa kudai kuwa WHO imeshindwa kukabiliana ipasavyo na mlipuko wa virusi vya Corona.

Mwezi uliopita, Rais Donald Trump alisema Washington inakata uhusiano na WHO kwa kudai kuwa shirika hilo lenye makao yake mjini Geneva lilikuwa linaitetea sana China. Hata hivyo, vitisho vyake vinaonekana vilikuwa vya maneno tu kwani bado hajaandika rasmi kwa shirika hilo la Umoja wa Mataifa.

Marekani ndio mfadhili mkubwa wa WHO ikichangia zaidi ya dola milioni 400 za kimarekani kwa shirika hilo mnamo mwaka 2019. Kiasi hicho cha fedha ni takriban asilimia 15 ya bajeti ya WHO.

Waziri wa afya wa Ujerumani Jens Sphan amesema kuwa euro milioni 500 iliotoa Ujerumani ndio kiasi kikubwa cha fedha ambacho Berlin imewahi kutoa kwa shirika la afya duniani.

Sphan amesema "Nina furaha kutangaza kuwa serikali ya shirikisho la Ujerumani inaiunga mkono WHO, kwa hiyo inatoa nyongeza ya Euro milioni 41 kwa ajili ya kulisaidia shirika hilo kutelekeza wajibu wake wa msingi hadi mwaka 2023. Pia, tunatoa nyongeza ya Euro milioni 25 kwa ajili ya utekelezaji wa mpango wa kimkakati"

Ufaransa imesema itatoa Euro milioni 90 kwa WHO

Schweiz Jens Spahn und Tedros Adhanom Ghebreyesus
Waziri wa afya wa Ujerumani Jens Sphan akiwa na mkurugenzi wa WHO Tedros Adhanom GhebreyesusPicha: Getty Images/AFP/F. Coffrini

Nayo, Ufaransa imesema itatoa kiasi cha Euro milioni 90 ili kufadhili kituo cha utafiti cha WHO kilichoko mjini Lyon. Nchi hiyo pia imesema itaongeza mchango mwengine wa Euro milioni 50.

"Ninaamini kuwa dunia inahitaji shirika la kimataifa litakalokuwa na ushirikiano wa mataifa mbalimbali. Tunahitaji jawabu dhidi ya ugonjwa wa Covid 19 na WHO pekee ndiyo inayoweza kupata jibu hilo," amesema waziri wa afya wa Ufaransa Olivier Veran.

Hata hivyo kwa upande mwengine, serikali za nchi za Ulaya zinafanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na Marekani ili kuweka mipango ya kulifanyia mabadiliko shirika hilo la afya duniani, alisema wiki iliyopita afisa mmoja wa afya wa ngazi ya juu barani Ulaya.

Tamko la afisa huyo wa afya linaashiria kuwa Ulaya pia una wasiwasi kama ilio nao Maarekani juu ya utendakazi wa WHO.

 

Chanzo: Reuters