Ujerumani: Mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano yavunjika | Matukio ya Kisiasa | DW | 20.11.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Ujerumani: Mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano yavunjika

Mazungumzo ya kuunda serikali ya mseto wa vyama nchini Ujerumani yamevunjika, baada ya chama cha Free Democrat- FDP kujiondoa, kikisema hakuna msingi wa makubaliano uliofikiwa baada ya wiki kadhaa za mashauriano.

Deutschland Angela Merkel Scheitern der Sondierungsgespräche (Getty Images/S. Gallup)

Kansela Angela Merkel amesema atamuarifu Rais wa Shirikisho kuhusu kuvunjika kwa mazungumzo ya kuunda serikali ya mseto wa vyama

Kuvunjika kwa mazungumzo hayo kati ya chama cha Angela Merkel cha Christian Democratic Union (CDU/SCU)  na vyama vya Free Democrat (FDP) na cha Walinzi wa Mazingira, (Die Grüne) kumeiacha Ujerumani kwenye njia-panda kisiasa.

Baada ya kujiondoa kwa FDP, Kansela Angela Merkel amesema amesikitishwa na mkwamo huo, lakini akaahidi kuipitisha salama Ujerumani katika kipindi kigumu cha siku za usoni.

Akizungumza na waandishi wa habari usiku wa manane leo, Bi Merkel amesema kwa kuzingatia heshima zote kwa chama cha FDP kilichojiengua katika mazungumzo, anasikitika kwamba hakuna muafaka uliopatikana.

 Berlin Lindner während der Sondierungsgespräche (Reuters/A. Schmidt)

Mkuu wa chama cha FDP Christian Lindner asema ''bora kukosa uongozi kuliko kuongoza vibaya'.

Lindner: Kila chama kina haki ya kung'ang'ania msimamo wake

Awali, kiongozi wa chama cha FDP Christian Lindner alitangaza kujiondoa katika mchakato huo wa kuunda serikali ya mseto iliyopachikwa jina ''Jamaica'', kutokana na rangi za bendera za vyama ambavyo vingeiunda, akisema, ''ni vyema kutokuwa katika uongozi, kuliko kuongoza vibaya.''

Lindner amesema chama chake hakikilaumu chama chochote kingine kwa kushikilia misimamo inayoendana na maadili yake, kwa sababu wao pia wamefanya hivyo.

''Tulichaguliwa kwa ahadi ya kubadilisha mkondo wa mambo ulivyo hivi sasa, lakini hatukufikia makubaliano,'' amesema Christian Lindner.

Hatima ya Angela Merkel mashakani

Ingawa Bi Angela Merkel ataendelea kukaimu katika nafasi ya ukansela, haifahamiki anabakiwa na chaguo gani tena la kuweza kuunda serikali mpya. Chaguo mojawapo ni kuendelea na mazungumzo na chama cha walinzi wa mazingira, Die Grüne, na kuunda serikali ya walio wachache bungeni. Jingine ni kujaribu kukishawishi cha ma SPD kilichokuja katika nafasi ya pili, kubadilisha mawazo na kuungana naye tena katika serikali ya muungano.

Hata hivyo, baada ya kushindwa vibaya katika uchaguzi wa Septemba, SPD kimesisitiza hakitaki tena kuingia katika serikali inayoongozwa na Bi Merkel, kikitaka kuongoza kambi ya upinzani bungeni. Ikiwa yote mawili yatashindikana, uwezekano wa uchaguzi mpya mwakani utakuwa ukibisha hodi.

Bi Merkel amesema atamuarifu leo rais wa shirikisho, Frank-Walter Steinmeier ambaye ana mamlaka ya kuitisha uchaguzi mpya ikiwa mchakato wa kuunda serikali ya mseto umegonga mwamba.

Mwandishi: Daniel Gakuba/ape,afpe,dpae, rtre

Mhariri:

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com