Uingereza kuchunguza ripoti ya dawa za kuongeza misuli nguvu | Michezo | DW | 04.04.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Uingereza kuchunguza ripoti ya dawa za kuongeza misuli nguvu

Serikali ya Uingereza imeitisha kuanzishwa uchunguzi baada ya ripoti moja ya gazeti kudai kuwa daktari mmoja wa London aliwatibu zaidi ya wanamichezo nyota 150 kwa kutumia dawa za kuongeza nguvu mwilini

Video ya siri iliyotolewa na gazeti la Uingereza la Sunday Times ilimwonyesha Daktari Mark Bonar akizungumza kuhusu kuwapa wanamichezo wa kulipwa – wakiwemo wachezaji wa Premier League, waendesha baiskeli wa Uingereza katika mbio za Tour de France, wachezaji wa Tennis na bondia wa Uingereza – na virutubisho vya mwili vilivyopigwa marufuku.

Waziri wa Michezo wa Uingereza John Whittingdale ameitisha uchunguzi wa dharura baada ya kuibuka kuwa Shirika la Uingereza la Kupambana na Matumizi ya Dawa za Kuongeza Misuli Nguvu – UKAD kwanza lilifahamu kuhusu madai hayo miaka miwili iliyopita lakini halikuchukua hatua wakati huo.

UKAD ilisema ingeweza tu kuwachunguza wanamichezo na maafisa ambao wanajumuishwa katika shirika hilo. Vilabu vikuu vya England, vikiwemo Leicester City Chelsea na Arsenal vimekanusha vikali madai hayo baada ya kutajwa katika ripoti hiyo.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/reuters
Mhariri:Yusuf Saumu