Uhispania yaipa masharti Catalonia | Matukio ya Kisiasa | DW | 11.10.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Uhispania yaipa masharti Catalonia

Waziri Mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy amewataka viongozi wa jimbo la Catalonia, kueleza bayana iwapo wamejitangazia uhuru, kabla serikali kuu ya mjini Madrid haijachukua hatua za kubatilisha mamlaka ya jimbo hilo.

Mariano Rajoy 29.9.2014 Porträt (picture alliance/dpa/Angel Diaz)

Waziri Mkuu wa Uhispania, Mariano Rajoy

Uamuzi huo Waziri Mkuu Mariano Rajoy ameutangaza baada ya kikao cha faragha cha baraza la mawaziri na baadaye atalihutubia bunge la kitaifa. Haya yanafuatia tangazo la Rais wa jimbo la Catalonia Carles Puigdemont,  aliyetangaza jana jioni kuwa ataendelea na mchakato wa kutangaza uhuru wa jimbo lake, lakini akasema hatua hiyo itacheleweshwa kwa wiki chache, ili kutoa nafasi kwa mazungumzo. Puigdemont alisema kucheleweshwa huko kulikuwa na lengo la kuzingatia ushauri wanaoupata kutoka viongozi wa nchi za Ulaya.

''Kuna rai kutoka Ulaya nzima, inayotaka mazungumzo, kwa sababu Ulaya tayari ina wasiwasi kuhusu kinachoweza kutokea ikiwa mzozo huu utamalizika vibaya. Sauti zote hizo zinapaswa kusikilizwa, na zote kwa ujumla wake zimetutaka kusubiri kwa muda ili mazungumzo na serikali ya Uhispania yawezekane.'' Alisema Puigdemont.

Uhispania yambeza Puigdemont

Spanien Parlament in Barcelona Carles Puigdemont (Getty Images/AFP/L. Gene)

Rais wa jimbo la Catalonia Carles Puigdemont akitangaza uhuru wenye utata

Lakini wito huo wa mazungumzo na serikali kuu ya Uhispania umekuwa kama kutwanga maji kwenye kinu. Serikali hiyo ya mjini Madrid haiitambui kura ya maoni ya tarehe 1 Oktoba, ambayo Puigdemont na viongozi wenzake wanaotaka kujitenga, wanaichukulia kama tukio la kihistoria, lililowapa mamlaka ya kujitangazia uhuru.

Naibu waziri mkuu wa Uhispania Soraya Saenz de Santamaria, amesema hakuna yeyote anayeweza kuwalazimisha kuingia katika majadiliano yasio halali.

''Sio bwana Puigdemont, wala yeyote mwingine, anaweza kutarajia kwamba - bila kufuata mkondo wa sheria na wa kidemokrasia, anaweza kutulazimisha kuzungumza. Mazungumzo ya kidemokrasia yanafanyika katika misingi ya sheria, yanafuata sheria, hakuna anayebuni sheria zake mwenyewe.'' De Santamaria amesema.

De Santamaria amemlinganisha Carles Puigdemont kama mtu asiyejua mahali alipo, wala anapotaka kuelekea.

Wakereketwa wa uhuru wakerwa

Spanien Demo für die Abspaltung in Barcelona vor der rede von Puigdemont (DW/A. Gumbau)

Wanaounga mkono uhuru wa Catalonia hawakufurahishwa na uamuzi wa kuuchelewesha uhuru huo

Baadhi ya wakazi wa mji mkuu wa jimbo la Catalonia, Barcelona ambao wanaunga mkono uhuru wa jimbo hilo, vile vile wameshangazwa na uamuzi wa kiongozi wao kusaini tangazo la uhuru, na kisha kuahirisha uamuzi huo.

Mmoja wao, Maria Rosa Bertran amesema hatua hiyo imewaweka katika hali mbaya zaidi, mithili ya kifo cha taratibu, tena chenye maumivu makali. ''Kubabaika katika maamuzi yetu, ndicho kitu kibaya zaidi kinachoweza kutusibu'', amesema.

Baada ya kutangaza uhuru wa Catalonia jana jioni, Puigdemont na washirika wake walilitia saini tangazo hilo nje ya chumba cha bunge, lakini uhalali wa tangazo hilo kisheria haueleweki. Mvutano huu unazidi kulididimiza jimbo hilo, na Uhispania kwa ujumla, katika mzozo unaozidi kupanuka.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe, ape

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com