1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Magari na usafirishajiUhispania

Ajali nyingine ya treni yaua na kujeruhi abiria Uhispania

Iddi Ssessanga dpae, ape,afpe
21 Januari 2026

Treni ya safari za mjini imepata ajali karibu na Barcelona, kaskazini-mashariki mwa Uhispania. Ajali hiyo imetokea siku chache baada ya treni ya mwendo kasi kupata ajali mbaya huko Andalusia na kuua watu 42.

https://p.dw.com/p/579cG
Uhispania, Gelida 2026 | Wahudumu wa uokoaji baada ya ajali ya treni iliyosababishwa na ukuta wa kingo (stützmauer) ulioporomoka
Treni ya abiria ya Uhispania iligonga ukuta wa kingo ulioporomoka, jambo lililosababisha ajaliPicha: Joan Mateu Parra/AP Photo/picture alliance

Mtu mmoja amefariki dunia na wengine 37 kujeruhiwa baada ya treni ya abiria wanaosafiri kila siku kupata ajali karibu na mji wa Barcelona kaskazini-mashariki mwa Uhispania, Jumanne usiku.

Kwa mujibu wa idara ya huduma za dharura, treni hiyo iligonga ukuta wa kingo ulioporomoka na kuangukia reli karibu na mji wa Gelida, takribani kilomita 35 nje ya Barcelona. Vyombo vya habari vya ndani viliripoti kuwa dereva wa treni alifariki katika ajali hiyo.

Majeruhi wapelekwa hospitalini

Idara ya huduma za dharura ya Catalonia ilisema watu 37 walijeruhiwa, watano kati yao wakiwa katika hali mbaya. Takribani ambulansi 20 zilitumwa eneo la tukio, na majeruhi kupelekwa katika hospitali tatu za karibu.

Idara ya zimamoto ya Catalonia ilithibitisha kuwa hakuna mtu aliyebaki ndani ya treni, huku operesheni ya kukagua chini ya treni na eneo la tukio ikiendelea ili kuhakikisha hakuna waathiriwa wengine.

Shirika la reli la Uhispania, ADIF, lilisema kuwa ukuta huo huenda uliporomoka kutokana na mvua kubwa iliyolikumba eneo la kaskazini-mashariki mwa nchi wiki hii. Huduma za treni za abiria zimesitishwa kwenye njia hiyo.

Ajali hiyo ilitokea kwenye njia ya R4 ya mtandao wa Rodalies, ambao kwa kawaida huwa na msongamano mkubwa wa wasafiri nyakati za jioni siku za kazi.

Ajali nyingine ya treni Catalonia

Katika tukio jingine siku hiyo hiyo, treni ya abiria ya Rodalies kwenye njia ya R2 iliondoka kwenye reli karibu na mji wa Blanes, baada ya mawe kuanguka kwenye reli kufuatia dhoruba kali. Hakuna majeruhi walioripotiwa, lakini huduma kwenye njia hiyo pia zimesitishwa.

Mamlaka pia zilithibitisha kupatikana kwa mwili wa mwanaume aliyesombwa na mafuriko karibu na mji wa Palau-Sator, baada ya gari lake kubebwa na maji katika mkondo ambao kwa kawaida huwa mkavu.

Kutokana na dhoruba kali iitwayo Harry, mamlaka zilitangaza tahadhari ya juu katika baadhi ya maeneo ya Catalonia, huku upepo mkali wa hadi kilomita 80 kwa saa na mvua kubwa zikiripotiwa. Wananchi walionywa kuepuka fukwe na bandari kutokana na mawimbi makubwa.

Uhispania, Córdoba 2026 | Kazi za uokoaji baada ya ajali mbaya ya treni iliyosababisha vifo vya angalau watu 41
Idadi ya vifo katika ajali ya treni ya mwendo kasi ya Jumapili imeongezeka na kufikia 42.Picha: Burak Akbulut/Anadolu/picture alliance

Idadi ya vifo yaongezeka Andalusia

Wakati huo huo, mamlaka za kusini mwa Uhispania zimeripoti kuongezeka kwa idadi ya vifo kufuatia ajali ya treni ya mwendo kasi iliyotokea Jumapili kati ya treni mbili karibu na mji wa Adamuz katika eneo la Andalusia.

Idadi ya vifo sasa imefikia 42 baada ya miili mingine mitatu kupatikana ndani ya mabehewa, mamlaka za eneo zilisema. Watu 10 pekee ndio waliotambuliwa hadi sasa, huku hofu ikitanda kuwa idadi hiyo huenda ikaongezeka zaidi.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Fernando Grande-Marlaska, aliliambia shirika la utangazaji la serikali RTVE kuwa watu 43 bado wanahesabiwa kuwa hawajulikani walipo. Polisi wanatumia mbwa maalum wa ufuatiliaji kuendelea na operesheni ya uokoaji.

Ajali hiyo mbaya iliondoa mabehewa mawili ya mbele ya treni moja kutoka kwenye reli na kuyatupa kwenye mteremko wa mita nne, huku baadhi ya miili ikipatikana umbali wa mamia ya mita kutoka eneo la ajali, kulingana na Rais wa Andalusia Juanma Moreno.