1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhasama mpya huko Gaza

Saumu Mwasimba28 Julai 2008

Wanajeshi wa Fatah wamewakamata wanachama 50 wa Hamas

https://p.dw.com/p/ElAj
Rais Mahmoud Abbas (kulia) akiwa na waziri mkuu wa zamani wa Palestina Ismail Haniyeh kabla ya uhasama mpya kuzuka.Picha: AP

Taarifa zinasema wanajeshi watiifu kwa Bw Abbas na chama chake cha Fatah ambacho kimo katika mapambano ya kuwania mamlaka ya kiutawala na chama cha Hamas katika ukanda wa Gaza baada ya Hamas kutwaa madaraka kwa nguvu Juni mwaka jana,wamewatia nguvuni zaidi ya wanaharakati 50 wa Hamas.

Hatua hiyo imechukuliwa huku hali ya wasi wasi ikizidi baada ya miripuko ya mabomu katika ukanda wa Gaza siku ya Ijumaa kuwauwa wanaharakati watano wa Hamas na mtoto mmoja wa kike.

Zoezi hilo lilianza usiku wa manane jana hadi asubuhi ya leo huku miongoni mwa waliokamatwa kwa mujibu wa maafisa wa Hamas wakiwa ni wahadhiri wa na wanafunzi wa chuo kikuu cha al Najah pamoja na madiwani wa mji huo, wafuasi wa chama hicho.

Hapo jana maafisa wa usalama wa Bw Abbas waliwakamata wanaaharakati 20 wa hamas katika mji wa Jenin na wengine 15 huko Tulkram.

Hatua hiyo inaonyesha ni ya kulipizana kisasi baada ya Hamas kwa upande wake kuwakamata jumla ya maafisa na wanaharakati 200 wa chama cha Fatah, tangu miripuko ya mabomu Ijumaa iliopita katika ukanda wa Gaza.

Chama hicho kinakitwika dhamana ya miripuko hiyo chama cha Fatah .

Leo hii maafisa wa Hamas wameyazuwia magazeti matatu makubwa ya Kipalestina kuingia eneo hilo, kikisema yanamafungamano na Fatah.

Akizungumzia juu ya kuzidi kwa mvutano kati ya pande hizo mbili, afisa wa ngazi ya juu wa Hamas Mahmud al Sahar alisema:-

"Hatukubali watu wetu kuuwawa na waisraili au washirika wao. Iwapo watashambuliwa na Abu Mazan au wengine au chama cha Fatah au kingine."

Kwa upande wake Rais Abbas amerudia tena wito wa kuwepo na mazungumzo na Hamas ambacho kilishinda wingi wa viti katika uchaguzi wa bunge 2006, na kutaka paundwe kamati huru ya wapalestina kuchunguza hujuma za Ijumaa iliopita.

Wakati huo huo, jumuiya mbili za haki za binaadamu zinasema pande zote mbili katika ukanda wa gaza na ukingo wa magharibi zimekua na mtindo wa kuwatesa wafungwa.

Shirika la Human Rights Watch lenye makao yake makuu mjini Newyork limesema kamata kamata kwa misingi ya kisiasa ni mambo yanayoendelea tangu Hamas ilipotwaa madaraka katika Gaza zaidi ya mwaka mmoja uliopita.

Nayo jumuiya ya kipalestina ya Al Haq imeripoti leo kwamba kiasi ya asilimia 20 hadi 30 ya wafungwa zaidi ya 20.000 elfu waliokamatwa mwaka jana wamekua wakipigwa na kugeuzwa pia wahanga wa visa vyengine vya ukandamizaji.

wakati mvutano na hali ya wasi wasi ikizidi miongoni mwa wapalestiana, Rais Husni Mubarak wa Misri amesema nchi yake itawaalika wawakilishi wa makundi ya wapalestina hivi karibuni, kwa vikao kadhaa vya majadiliano mjini Cairo.

Hata hivyo juhudi za awali kujaribu kuyapatanisha makundi hayo zimeshindwa kuzaa matunda.