Uganda kuanza mradi wa uchimbaji mafuta hivi karibuni | Masuala ya Jamii | DW | 18.11.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Uganda kuanza mradi wa uchimbaji mafuta hivi karibuni

Wakati Uganda mwaka huu inajiandaa kuelekeza nguvu kubwa katika uchimbaji mafuta, huko upande wake wa magharibi, lakini bado inakosolewa kwa kutofanya jitihada za kutosha mpaka sasa, katika uchimbaji wa madini.

Bendera ya Taifa ya Uganda

Bendera ya Taifa ya Uganda

Wakati Uganda mwaka huu inajiandaa kuelekeza nguvu kubwa katika uchimbaji mafuta, kwenye eneo la karibu na mpaka wake kwa upande wa magharibi wa nchi hiyo, lakini bado inakosolewa kwa kutofanya jitihada za kutosha mpaka sasa, katika uchimbaji wa madini kwenye maeneo kadhaa yenye hifadhi ya kutosha ya rasilimali hizo.

Mkurugenzi Mkuu wa taasisi ya udhibiti wa nishati kwa Afrika, Dickens Kamugisha akiongea na shirika la habari la IPS amesema, rasilimali hizo hazijawekezwa ya kutosha, ambapo ingeweza kuwa ni kitega uchumi kizuri na kukuza soko la ajira nchini humo, hasa katika maeneo yenye hifadhi hizo kwa wingi na bado yamekithiri kwa hali ya umasikini.

Ushuru wa Rasilimali peke yake, kuweza kubeba uchumi wa Uganda

Kamugisha aliongeza kuwa, ushuru peke yake kutokana na utajiri wa rasilimali hizo, ungeweza kutosheleza kubadili na kukuza hali ya uchumi wa nchi hiyo, kuboresha huduma za kijamii na kumaliza mapambano ya kukabiliana na umasikini pamoja na magonjwa yanayosababishwa na ufukara.

Kijana wa Kiganda anayesumbuliwa na maradhi kutokana na ufukara

Kijana wa Kiganda anayesumbuliwa na maradhi kutokana na ufukara

Uganda ina utajiri wa hifadhi ya rasilimali nyingi kama dhahabu, shaba, kobalti na uraniam, ambapo Mwaka 2006 kiasi kikubwa cha hifadhi ya rasilimali ya mafuta, kiligunduliwa katika eneo lililopo karibu na ziwa Albert huko magharibi mwa nchi hiyo, eneo la mpakani na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Ingawaje ripoti ya mwisho ya maendeleo ya malengo ya milenia kwa mwaka 2013 ya Uganda, iliyotolewa mwezi Oktoba ilionyesha kuwa, kati ya mwaka 1990 hadi mwaka 2010, umaskini nchini humo umepungua kutoka asilimia 50 hadi kufika asilimia 24.5. Ripoti hiyo inatofautiana na mtazamo wa hali halisi, ambapo umaskini bado umeshamiri kwa kiwango kikubwa katika maeneo kadhaa vijijini na ndio kuna idadi kubwa ya watu wanaokadiriwa kuwa asilimia 85 ya idadi ya watu wa nchi nzima.

Umaskini kutokana na nguvu haba ya kufyonza rasilimali

Klimakrieg in Karamoja Timothy Stammesführer

Mtu wa kabila la karamoja nchini Uganda,eneo la mafuta

Mchambuzi wa masuala ya sera nchini Uganda, Onesmus Mugyenyi, alipozungumza na shirika la habari la IPS, amesema kiwango cha umaskini wa nchi hiyo, unatokana na kushindwa kuwekeza nguvu ya kutosha kwenye rasilimali walizonazo na kuongeza kuwa, wakazi wa vijijini nchini humo, wanaishi kwa kutegemea shughuli zitokanazo na rasilimali zilizowazunguka, hasa ardhi katika kilimo, hivyo basi ukuzaji wa matumizi ya rasilimali zilizopo ni nje ya jitihada za serikali hiyo katika kupunguza kiwango cha umasikini nchini humo.

Mugyenyi amesema, nchi hiyo ina sera nzuri za uwekezaji na uchimbaji wa rasilimali zilizopo,lakini hazijapata msukumo katika utekelezaji.

Waziri wa madini nchini Uganda, Peter Lokeris naye alipozungumza na shirika la habari la IPS amesema, nchi yake kimsingi haina uwezo wa kutosha katika kuchimba kiasi kikubwa cha rasilimali walizonazo za madini na mafuta, kwani kazi ya uchimbaji madini inahitaji utaalamu mkubwa na uwezo mkubwa wa kifedha. Aliongeza kusema kwamba kwa sasa, serikali yake imeshaandaa sheria na uwezo wa kuanza uchimbaji wa madini walizonazo.

Watu kabila la Karamoja waliopo upande wa kaskazini Magharibi wa Uganda, eneo lenye utajiri mkubwa wa rasilimali hizo, zipatazo karibu aina 50 tofauti wa kabila la Karamoja waliopo upande wa kaskazini Magharibi wa Uganda, ndio wanaongoza katika kundi la watu wenye umaskini uliokithiri nchini humo, ambapo takwimu za nchi hiyo zinaonyesha,asilimia 82 ya watu wa kabila hilo wapo katika umasikini, na asilimia 8 tu ndio walau wapo katika hali nafuu kidogo.

Mwandishi: Diana Kago/IPS
Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com